Chadema yatangaza mikutano ya hadhara
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza kuanza mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali nchini licha ya serikali kupiga marufuku kufanyika mikutano ya aina hiyo.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, alitangaza kuanza kwa mikutano hiyo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu maazimio ya kikao maalum cha Kamati Kuu ya chama hicho iliyokutana kwa siku mbili jijini kuanzia Februari 9.
Alisema Chadema kinaanza kufanya mikutano ya hadhara baada ya kukamilisha mambo yake ndani ya chama.
Dk. Mashinji alisema kinachoendelea kwa sasa ni uratibu na utengenezaji wa ratiba itakayowaongoza maeneo ya kufanya mikutano hiyo.
"Kufanya mikutano ya hadhara siyo jinai na hata aliyezuia aliizuia kwa utashi, siyo kwa msukumo wa kisheria. Ni kweli, hata sisi tulikuwa na mambo ya ujenzi wa taasisi, kwa hiyo hatukuwa na uwezo wa kufanya vitu viwili kwa wakati mmoja,” alisema.
Aliongeza kuwa: "Kufanya mikutano ya hadhara, kukimbizana na uchaguzi wetu wa ndani, kukimbizana na majukumu ya kiutawala, kukimbizana na mifumo ya uchaguzi ndiyo maana tamko la kuzuia mikutano ya hadhara lilipotoka ilionekana kana kwamba tumetii amri isiyo halali.
“Tunawataka wapenda demokrasia wote duniani, kwanza kupinga hii mifumo isiyo ya kidemokrasia, kupinga kuingilia uhuru wa watu binafsi na uhuru wa taasisi zilizo huru.
“Tunajua wanajificha kwenye kichaka cha kwamba Chadema tunatumia mikutano ya hadhara kutukana watu na kuwadhalilisha, sisi huo muda mchafu hatuna, tuna sera zetu ambazo tunataka wananchi wazitambue.
"Tuna kazi kubwa ya kueneza sera zetu kuanzia mijini hadi vijijini, kwa hiyo hatuna muda mchafu wa kuongelea watu walioshindwa kutekeleza yale waliyoyaomba kikatiba."
Rais John Magufuli ameshatangaza kuwa serikali anayoiongoza haitaruhusu maandamano na mikutano ya hadhara nchini, isipokuwa mikutano inayofanywa na wabunge na madiwani kwenye maeneo waliyochaguliwa.
UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA
Dk. Mashinji pia alizungumzia uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajia kufanyika Agosti, akieleza kuwa Kamati Kuu ya Chadema imependekeza mambo mawili.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni uchaguzi huo kusimamiwa na tume huru ya uchaguzi badala ya Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na kuboreshwa kwa daftari la kudumu la wapigakura.
“Tulikuwa na rejea ya kanuni zinazosababisha uendeshaji wa uchaguzi, kuna mambo ya msingi ambayo kwenye Kamati Kuu tumeyajadili na kuyapitishia uamuzi na maazimio, tunapenda Watanzania wajue na serikali ijipange," alisema.
Kiongozi huyo wa Chadema alisema Kamati Kuu ya chama hicho imeazimia kuitaka serikali ihakikishe daftari la kudumu la wapigakura linatumika katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
"Kwa lugha nyingine, hii inapeleka msukumo wa kisheria kuhakikisha daftari hili linaboreshwa mara kwa mara kama sheria inavyotaka -- linatakiwa liboreshwe mara mbili katika kipindi cha miaka mitano, hadi sasa wanachi hawajaambiwa daftari hili litaboreshwa lini," alisema.
Dk. Mashinji alisema Kamati Kuu pia imependekeza uchaguzi huo usimamiwe na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kuwa ndiyo yenye dhamana hiyo na hawana sababu ya kukwepa kusimamia demokrasia ya nchi.
Awali Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Prof. Abdallah Safari, alisema kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kililenga kuzungumzia hali ya siasa nchini na ajenda ya kupambana na ufisadi nchini.
Alisema Kamati Kuu imeona mapambano dhidi ya ufisadi bado hayajafanikiwa, alitolea kutoonekana kwa matumizi ya Sh. Trilioni 1.5 katika taarifa za hesabu za serikali kwa mwaka 2016/17 kulikoibua mjadala mkali bungeni wakati wa Bunge la Bajeti lililopita. Prof. Safari alisema suala lingine ambalo Kamati Kuu
No comments