Breaking News

Serikali yatoa zaidi ya Bil.42 kwa ajili ya kukarabati shule kongwe




Serikali imetoa zaidi ya sh. bilioni 42 kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya Sekondari 42 kati ya shule 88 kongwe zilizopo nchini kote ikiwemo shule ya Sekondari ya Wasichana Ruvu iliyoko Wilayani Kibaha Mkoani Pwani.

Akizungumza mara baada ya kukagua ukarabati wa shule hiyo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango. Dkt. Ashatu Kijaji, amesema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa shule zote Kongwe ambazo zinahistoria kubwa ya kutoa viongozi wengi na wataalam mbalimbali nchini, zinakuwa na hadhi na kuwa kimbilio la wananchi.

Ametoa wito kwa uongozi wa shule hiyo ya Sekondari ya Wasichana Ruvu, kuhakikisha kuwa elimu bora inatolewa kwa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo ili thamani ya uwekezaji mkubwa wa Serikali unaofikia zaidi ya shilingi bilioni 990 uweze kuonekana

Kwa upande wao, Mbunge wa Kibaha Vijijini, Hamoud Juma na Mkuu wa Shule hiyo, Juliana Chimazi, wameishukuru Serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha shule hiyo na kuomba wapatiwe fedha kwa ajili ya kununulia samani hasa vitanda kwa ajili ya wanafunzi ili kwenda sambamba na uboreshaji mkubwa wa majengo uliofanyika shuleni hapo.

Miongoni mwa miundombinu iliyoboreshwa katika shule hiyo ya Sekondari ya washichana Ruvu ni pamoja na mifumo ya maji taka, madarasa, vyoo, mabweni, nyumba za walimu na Ofisi.

Naibu Waziri Dkt. Kijaji anaendelea na ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali iliyopewa fedha na Serikali ikiwemo ya kimkakati inayolenga kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kujitekemea kwa mapato.

No comments