Breaking News

WB yafurahishwa miradi ya maendeleo


SERIKALI imesema katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais John Magufuli, Benki ya Dunia imeshatoa zaidi ya shilingi trilioni mbili kwa ajili ya kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

Fedha hizo zimetumika katika miradi mitatu ya uendelezaji wa majiji, miji na Jiji la Dar es Salaam katika ujenzi wa miundombinu ya barabara, vituo vya mabasi, madampo na masoko katika mikoa mbalimbali nchini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, aliyaeleza hayo jana alipoongozana na maofisa kutoka Benki ya Dunia, walipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa Miradi ya Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam inayotekelezwa na wizara yake katika manispaa za Kinondoni, Ilala na Temeke.

Akiwa katika Manispaa ya Temeke alipotembelea ujenzi wa kituo cha afya cha Buza, Jafo alisema Benki ya Dunia imesaidia utekelezaji wa miradi itakayowezesha kukuza uchumi wa wananchi na maendeleo ya taifa.



“Namshukuru Rais John Magufuli katika kipindi cha uongozi wake tangu aingie madarakani, Benki ya Dunia imeshafadhili miradi mbalimbali ya maendeleo kwa gharama za Dola za Marekani bilioni moja, sawa na zaidi ya shilingi trilioni mbili, ambazo zimesaidia kutatua changamoto mbalimbali za maendeleo katika nchi yetu," Jafo alisema.

Alisema utekelezaji wa miradi hiyo unasimamiwa kwa karibu na Rais Magufuli katika kuhakikisha anatekeleza ahadi alizotoa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na lengo ni kuwaletea wananchi maendeleo.

Alitaja baadhi ya majiji na miji ambayo miradi hiyo inatekelezwa kuwa ni Tanga, Arusha, Ujiji, Mikindani na Mbeya zinakojengwa barabara za kisasa.

Maeneo mengine alitaja kuwa ni katika miji na manispaa katika mikoa mbalimbali nchini kwa kujenga stendi za mabasi na miundombinu kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.



Akikagua barabara ya Tuangoma iliyoko Mbagala wilayani humo, alimwagiza Mkuu wa Wilaya hiyo, Felix Lyaniva, kuhakikisha anasimamia usafi katika miradi hiyo, baada ya kuona takataka zimeshaanza kutupwa katika mitaro.

“Naagiza Mkuu wa Wilaya uhakikishe unaanzisha kampeni maalum ya kudhibiti uchafu katika miradi hii kwa sababu nimeshaona takataka zimeanza kutupwa kwenye mitaro hii. Suala la ujenzi ni jambo moja na jambo la msingi zaidi ni kuilinda miradi hii isiharibiwe," Jafo alisema.

Akiwa katika maeneo ya Mbagala Kuu na Kijichi, eneo la Tuangoma na Kijichi, Jafo alisema maeneo hayo yamebadilika kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka mitatu iliyopita kufuatia ujenzi wa miradi inayoendelea.

Alisema changamoto iliyokuwa katika mto Mzinga ya kuwagawa wakazi wa maeneo hayo imetatuliwa baada ya kujengwa daraja la kisasa pamoja na soko la kisasa Mbagala na Kijichi yatakayowezesha wakazi wake kupata bidhaa na soko la Kijichi litaufanya kuongeza thamani ya maeneo hayo.

Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Temeke, Abdallah Chaurembo, alisema wametekeleza vizuri miradi yote na kumwomba Rais Magufuli kuwapatia fedha za miradi mingine zaidi.

Alisema miradi hiyo inatekelezwa katika kata 13, lakini kuna kata nyingine ambazo zinahitaji fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Benki ya Dunia kutoka Makao Makuu nchini Marekani, Sameh Wahba, alisema ameridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo katika Wilaya ya Temeke, inayotekelezwa kwa kushirikiana na viongozi wa serikali na watendaji wengine.

Pia alisema kwa kazi nzuri aliyoshuhudia hayupo katika nafasi ya kuahidi kuwa, Benki ya Dunia itaendelea kufadhili miradi mingine isipokuwa inaweza kuwa sehemu ya kuendelea kupata ufadhili.

No comments