Wasimamizi wa huduma za afya nchini watakiwa kusimamia uwajibikaji
Naibu Katibu Mkuu Afya, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Dkt. Dorothy Gwajima amewagiza waratibu wa timu za usimamizi huduma za afya Mikoa (RHMT) na Halmashauri (CHMT) nchini kuhakikisha, wameimarisha mifumo ya uwajibikaji ili kuleta mabadiliko katika sekta ya afya nchini.
Ameyasema hayo alipokuwa kwenye mwendelezo wa ziara zake za kikazi kwa lengo la kukagua uwajibikaji wa timu hizi kwa Mkoa wa Dodoma katika kituo cha afya cha Bahi kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Jijini Dodoma.
Dkt. Gwajima amesema, zoezi la kuwapima uwajibikaji limeanzia Mkoani Dodoma likiwa ni endelevu ambapo ndani ya siku 90 litakuwa limekamilika nchi nzima ambapo wale wote wasiopenda kubadilika watapangiwa majukumu mengine wanayoyamudu.
“Hakuna haja ya kila siku semina, washa, mikutano halafu ukienda vituoni, mambo ya kawaida kabisa unakuta hayako vizuri wala takwimu hakuna na hakuna maelezo yoyote yenye mashiko kwa nini hali imekuwa hivyo ilivyo” Amesema Dkt. Gwajima.
Dkt. Gwajima amesema, pamoja na kazi nzuri zinazofanywa katika baadhi ya maeneo, yapo masuala ya msingi ambayo, yanahitaji kusimamiwa vizuri zaidi na na hayahitaji chochote cha ziada zaidi ya uwajibikaji imara wa viongozi waliopewa dhamana.
Dkt. Gwajima amesema, Serikali haitavumilia kuwa na waratibu ambao, hawaleti msukumo katika kuleta mabadiliko ya uwajibikaji na badala yake wamebaki kusafiri na kuhudhuria semina, washa na mikutano ambayo haileti tija katika maeneo yao ya kazi.
“Inasikitisha kuona baadhi ya waratibu wanahudhuria semina, mikutano na warsha mbalimbali lakini hakuna mabadiliko na wengine hukaa ofisini na hata wanapoenda kutembelea vituo hawaoni mapungufu na wakiyaona hawaandai mpangokazi wa kuboresha na wakiandaa mpangokazi hawafanyi ufuatiliaji bali, wanafungia taarifa kwenye makabatikatika utendaji kazi wa sasa” Anafafanua Dkt. Gwajima.
Aidha, amesema waratibu ambao wanashindwa kwenda na kasi ya usimamizi unaotakiwa enzi hizi, wajipime mapema kabla ya kupimwa na tayari mpaka sasa Dkt. Gwajima amewabadilisha waratibu kadhaa katika ziara zake baada ya kuona hawasimamii wajibu wao wa msingi bali wanajitetea zaidi kuliko kuonesha njia hata pale ambapo, hapahitaji fedha bali uwajibikaji tu.
“Wakati wa kusema bila takwimu umeisha. Kama umeingia kazini lazima useme umefanya nini? Kama ni wateja je, umehudumia wangapi siyo kulalamika tu watumishi hawatoshi, je umehudumia wateteja wengi kiasi gani kuzidi uwingi wa majukumu uliyowekewa kwa vigezo na takwimu? Uchache wa watumishi siyo namba bali ni sambamba na uwingi wa majukumu kwa takwimu zisizotia shaka.” Amesema Dkt. Gwajima
Dkt. Gwajima ameawaagiza waratibu kufanya usimamizi na ufuatiliaji kwa weledi mkubwa ambapo kila mmoja atatakiwa kuonyesha ameona nini na mpangokazi ni upi na umefanikisha ufumbuzi wa changamoto ngapi, kama umekwama je, umechukua hatua gani za kuomba msaada.
Kuhusu ushirikishwaji wa wadau Dkt. Gwajima amezielekeza timu hizo kuwa na Kamati za Afya za Vituo na Bodi za Afya ambazo, ni wawakilishi wa wananchi ziwezeshwe ili, kuimarisha kiungo kati ya kituo na wananchi wanaowakilishwa na Kamati hizi. Bila kiungo hiki muhimu kati ya vituo na wananchi ni dhahiri kuwa, tutakwama kwenda na kasi tunayohitaji.
Ametoa wito kwa timu za afya nchini kujifunza toka timu za Dodoma ambao, kwa kutumia fursa ya kuwa karibu na Wizara wameona kwa vitendo nini kinatakiwa ili, nao waanze mara moja kuimarisha mifumo na kuanza mbio za mabadiliko kabla zoezi la tathmini ya Wizara halijawafikia hivyo RHMT na CHMT zinahitajika kuwa imara ili, kuchochea huduma bora katika vituo vya tiba.
Dkt.Gwajima ameendelea kusisitiza kuwa, ni wakati wa kila aliyepewa dhamana kuvaa koti la uzalendo na kuakisi kwa vitendo mwendo wa Serikali ya awamu ya tano katika kuleta mabadiliko ya uwajibikaji kwa haraka.
Aidha, amewapongeza watumishi wote ambao, pamoja na changamoto ambazo zipo, wameendelea kupambana na kuleta mabadiliko na amewaasa kutokatishwa tamaa na wachache wasiopenda kubadilika maana, Serikali ina macho na Jamii pia ina macho na inatambua juhudi za kila mmoja na haitawavumilia wale ambao, wanarudisha nyuma kasi ya maendeleo.
Aidha ikumbukwe kuwa Dkt.Gwajima ameendelea kufanya ziara zake za kikazi za kukagua utendaji kazi wa vituo vya huduma za afya katika Jiji la Dodoma, Halmashauri ya Wilaya Chamwino na Halmashauri ya Wilaya Bahi na itahitimishwa kwa kuwa na kikao cha Wadau wote ili, kwa pamoja kujionea hali halisi ilivyo na kuwekeana mikataba ya kazi na uwajibikaji
Pata habari motomoto na za uhakika kila siku kila zinapojiri katika nyanja mbalimbali ikiwemo Siasa, Michezo, Ajira, uchumi, Mapenzi, Udaku/Umbea n.k .Kwa kudownload APP hii Bofya HAPA Kudownload.
BOFYA HAPA
No comments