WAZIRI NDALICHAKO ATAKA WANAWAKE KUSHIKAMANA NA KUSAIDIA MAKUNDI YA WATU WASIOJIWEZA
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako amewataka wanawake kuwa mstari wa mbele katika kusaidia makundi ya watu wasiojiweza hasa watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Prof Ndalichako ametoa wito huo mkoani Kigoma wakati akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya siku ya maombi ya dunia ya umoja wa wanawake wa kikristo Tanzania CCT na kusema kuwa wanawake wakiamua wana uwezo mkubwa wa kubadili maisha katika jamii.
Amesema wanawake ndio walezi wa watoto kuanzia ngazi za familia akiwafananisha na walimu kwani wao wana jukumu la kulea na kufundisha watoto wote.
“Wanawake wenzangu tukumbushane msemo ambao Mama Salma Kikwete ambae ni mke wa Rais Mstaafu wa awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amewahi kusema kuwa mtoto wa mwenzio ni wa kwako hivyo tuwasaidie watoto yatima, wa mitaani na wale wanaoishi katika mazingira magumu ili waweze kutimiza ndoto zao hasa za kupata elimu,” alisisitiza Waziri Ndalichako.
Pia, Waziri Ndalichako amewataka wanawake nchini kudumisha mshikamano miongoni mwao na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Mhe. Rais Dkt. John Magufuli kwa vitendo kwa kuhakikisha wanafanya shughuli mbalimbali za uzalishaji mali kwa lengo la kujipatia kipato.
Akiwa mkoani humo waziri Ndalichako pia aliwatembelea wagonjwa ambao wamelazwa katika hospitali ya rufaa ya Kigoma Maweni na kutoa misaada mbalimbali kwa wagonjwa hao.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
02/03/2019
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
02/03/2019

No comments