Breaking News

WAZIRI UMMY AKEMEA TABIA YA VIONGOZI KUWAWEKA NDANI WAUGUZI




WAMJW-Manyara

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Ummy Mwalimu amekemea tabia baadhi ya wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya nchini kuwaweka ndani wauguzi kutokana na tuhuma mbalimbali wanazokutana nazo wakiwa kazini.

Waziri Ummy amesema hayo mapema leo wakati akimuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wauguzi duniani ambayo kitaifa yamefanyika mkoani Manyara na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na mkoa huo.

Waziri Ummy amesema endapo muuguzi atatuhumiwa kufanya kitu ambacho siyo cha kitaaluma na maadili inatakiwa apelekwe kwenye mabaraza ya taaluma husika likiwemo baraza la wauguzi ili aweze kuchukuliwa hatua za kinidhamu kulingana na taaluma yake lakini siyo kumuweka ndani.

“Tunalo baraza la wauguzi na wakunga nchini Tanzania, kama unadhani muuguzi amekosea mpeleke kwenye baraza atachukuliwa hatua kwa kuzingatia miongozo na sheria za nchi na sio kwa matakwa ya kisiasa”. Amesema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy ameendelea kusisitiza kuwa taaluma ya uuguzi ina changamoto nyingi ikiwemo upungufu wa watumishi na vitendea kazi lakini wauguzi wanatumia muda mwingi kukaa na mgonjwa bila kujali changamoto wanazokutana nazo wakiwa kazini hivyo ni lazima waheshimiwe kwa kazi kubwa wanayofanya.

“Nimeongea na wauguzi wengi wa sehemu tofauti tofauti, wengi wao wanaumwa migongo kutokana na kazi wanayofanya. Utakuta muuguzi mmoja anafanya kazi ya wauguzi nane kwa wakati mmoja kwa hili inapaswa tuwaheshimu na kuwapa moyo”. Amesisitiza Waziri Ummy.

Katika maadhimisho hayo wauguzi mbalimbali walipewa vyeti na zawadi kwa kutambuliwa kuwa na mchango mkubwa katika maeneo yao ya kazi.

No comments