JICHO LA MWEWE: Simba inaharibiwa na mchawi huyu hapa
By Edo Kumwembe
PALE Simba kuna wachawi wengi. Mchawi mwingine ambaye wanatembea naye ni matazamio. Ijumaa walitupwa nje ya Michuano ya SportPesa pale Uwanja wa Taifa na ghafla mashabiki wakaigeuka timu. Wakamgeuka kila mtu klabuni.
Wa kwanza aliyesemwa sana alikuwa Kocha Patrick Aussems. Simba inapofungwa anatajwa kuwa hana mbinu. Simba ikishinda mashabiki wanakaa kimya. Ni maisha ambayo inabidi ayazoee katika Simba. Hata angekuwa Yanga ingekuwa hivyo hivyo.
Ghafla Simba wakamgeuka hata msemaji wao, Haji Manara. Jana alikuwa na sherehe yake binafsi pale Hayyat Hotel lakini mashabiki wa Simba wakamjia juu. Hawakuona umuhimu wa yeye kufanya sherehe yake binafsi wakati timu imefungwa. Vina uhusiano gani?
Tatizo kubwa la Simba ni matazamio ya mash abiki. Kikosi cha mabilioni ya pesa kinawa athiri kisaikolojia. Simba wanaona hawana ruhusa ya kufungwa na timu yoyote ile. Hata mechi dhidi ya Vita Simba hawaujajadili sana ubora wa Vita. Wamejadili zaidi mapungufu yao. Hawaijui safari yao ya kufikia uimara wa Vita ilivyo ndefu.
Rafiki yangu Haji Manara naye ana mchango wake katika hili. Kwa kiasi kikubwa amesaidia sana kuwahamasisha mashabiki wa Simba kuipenda timu yao. Ni kitu kizuri. Maneno yake yanawapeleka mashabiki wa Simba uwanjani au yanachangia kwa kiasi kikubwa mashabiki kugandisha macho yao katika televisheni. Wanachosubiri mashabiki ni ushindi tu. Hakuna mbadala wa matokeo hayo.
Simba wanapojifikiria kwamba wana Emmanuel Okwi, Clatious Chama, John Bocco, Meddy Kagere, Jonas Mkude na wengineo hawaoni kama kuna timu ya kuwafunga duniani. Wao wanaitazama timu yao hivyo, mimi naitazama kama timu ambayo inahitaji kuimarika zaidi na zaidi.
Kwa soka la ndani maisha yanaweza kuwa rahisi, kwa soka la nje maisha ni tofauti. Nani alijua Simba ina mapungufu makubwa katika mipira ya kutengwa? Vita walifunga mabao mawili ya vichwa wakiwa huru. Bandari walitawala hivyo hivyo mipira ya juu. Mbeya City au Alliance haziwezi kutuonyesha mapungufu ya Simba.
Ni wakati wa Haji na baadhi ya mabosi wa Simba kuelewa ukweli na kuwaeleza mashabiki Simba ipo katika mchakato wa kurudi kutamba kimataifa. Haiwezi kuwa kwa msimu mmoja. Soka ni mchakato ambao Tanzania hatutaki kuupitia.
Ghafla ndani ya msimu mmoja mashabiki wameiona ni timu ambayo inaweza kucheza na Barcelona au Manchester City bila ya wasiwasi. Achilia mbali maneno ya Haji lakini mechi dhidi ya Mbabane Swallows na Nkana zimepaisha matumaini kupitiliza.
Mashabiki wamesahau kuna maeneo ambayo Simba inabidi yafanyiwe kazi. Wamesahau klabu kama Vita au zile za Afrika Kaskazini ambazo zinashiriki michuano ya Afrika zina wachezaji walionunuliwa kwa dau la Pauni 500,000, wengine wamenunuliwa dau la Pauni milioni moja.
Simba imefikia kiwango hiki cha uwekezaji? Bado haijafika. Haina biashara ya mpira ambayo inaifanya kiasi cha kufikia kuwekeza kiasi hiki. Wale kina Al Ahly wanawekeza kwa sababu wanajua ni biashara inayoweza kulipa kama ukitwaa ubingwa wa Afrika. Lakini pia wana makampuni makubwa ambayo yanawaingizia pesa.
Simba inaweza kuifunga Al Ahly au kama vile walivyoifunga Nkana lakini haitoi majibu ya jumla kwamba ipo juu ya hao.
Mfano mwingine ni ule wa Ijumaa. Nimetazama soka la timu za Kenya ambazo nyingi hazina wachezaji wa kigeni, ukweli ni kwamba mpira wao upo juu kuliko huu mpira wetu. Ingeweza kutokea Simba kuifunga Bandari au Gor Mahia, ingeweza kutokea Yanga kuifunga Gor Mahia au Bandari au AFC Leopards lakini ukiwatazama mchezaji mmoja mmoja ndani ya uwanja unaweza kuelewa wachezaji wa Kenya wanachofanya uwanjani kuliko wachezaji wetu.
Bahati nzuri ambayo imeibeba timu kama ya Simba katika mechi dhidi ya Leopards ni uwepo wa wachezaji wa kigeni ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa nguzo kubwa kwa Simba ya sasa.
Vinginevyo kama ingekuwa mechi ya wazawa watupu nadhani Simba ingeangukia patupu katika mechi ile.
Sio mechi ile tu, sioni kama Simba ingefuzu hata hatua ya makundi bila ya kina Chama na Kagere. Wote tumeona walichofanya. Lakini kwa ujumla soka letu na lile la Kenya bado ni vitu tofauti. Sio Kenya tu, hata Uganda.
Mashabiki wa Simba wapunguze matumaini yaliyopitiliza kwa timu yao. Ukitaka kujua ni namna gani mashabiki wamekuwa na matumaini yaliyopitiliza ni pale ambapo wamekuwa wakimlaumu zaidi kocha kuliko wachezaji. Wanaamini wana wachezaji ambao wanaweza kuwapatia ubingwa wa Afrika. wanaamini wana wachezaji ambao wanaweza kuifunga Bayern Munich kama Haji alivyosema. Sio kweli, timu yao bado ipo katika mchakato. Bado inaanzia chini kwenda juu. Hata kwa Simba kutinga katika hatua ya makundi michuano hii ya CAF ni mafanikio tosha.

No comments