Breaking News

KAKOBE:CHADEMA ITAANGAMIA,AWATAKA KUTUBU HADHARANI KWA KUWAKEJELI VIONGOZI WA DINI.



Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zacharia Kakobe amesema Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimo shimoni na endapo viongozi wake hawatatubu kwa kuwakejeli viongozi wa dini, chama hicho “kitadumbukia kwenye shimo refu zaidi na hakitaweza kuinuka tena.”

Hayo aliyasema jana jijini Dar es Salaam katika Ibada ya Jumapili iliyofanyika katika kanisa lake lililopo maeneo ya Sinza ambapo alitumia ibada hiyo pia kukanusha mambo mbalimbali aliyodai hayana ukweli wowote.

Januari 23 mwaka huu zaidi ya viongozi 100 wa dini mbambali walikutana Rais Dk. John Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam na kufanya mazungumzo nao kuhusu mambo mbalimbali yanayoendelea nchini huku wakimpongeza na kutoa changamoto na maoni kuhusu changamoto hizo.

Kutokana na mkutano huo viongozi wa Chadema kwa nyakatitofauti walitumia mitandao ya kijamii kujadili mkutano huo na kuishia kuwakejeli viongozi hao wa kiroho.

Askofu kakobe alisema kuhudhuria kwake mikutano ya Rais Magufuli kumeibua mitazamo tofauti ikiwemo watu kusema kuwa ameahidiwa ubunge huku wengine wakidai amenunuliwa.

“Mimi nitanunuliwa shilingi ngapi? Si wanafahamu nilisema nina pesa kuliko serikali na TRA walipokagua akaunti yangu wakatangaza kuna hela za kanisa za kutosha? Sasa nitanunuliwa kwa bei gani mimi sina bei,” alisema Askofu Kakobe huku waumini wake wakishangilia.

Aidha Askofu Kakobe alikanusha kuwa yeye si mwanasiasa na wala hajawahi kuwa mwanachama wa Chadema licha ya kuwahi kuhudhuria mkutano wao si kama mwananchama bali kama baba ambaye anaweza kualikwa na watoto wengi.

Alisema hajawahi kukutana na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na wala kuwa na mazungumzo naye kwa njia ya simu na kwamba alihudhuria mkutano huo uliofanyikia Mlimani City alipokewa na viongozi wengine.

Aidha alikanusha kuwahi kuonana au kuongea kwa njia ya simu na Mbunge wa Ubungo Said Kubenea, ambaye anaongoza eneo lilipo kanisa lake.

“Mimi nimehudhuria mikutano mingi ya CCM kuliko Chadema nakumbuka niliwahi kuhudhuria mkutano wa wazee kumuaga Rais Benjamin Mkapa nikiwa nimealikwa na Yusuph Makamba na nlikua nahudhuria mikutano mingi kwasababu alikuwa rafiki yangu,” alisema

No comments