YALIYOJIRI KATIKA KIKAO CHA MAJUMUISHO CHA MAWAZIRI KUTOKA TANZANIA NA UGANDA WANAOHUSIKA NA UTEKELEZAJI WA MRADI WA BOMBA LA MAFUTA GHAFI KUTOKA UGANDA HADI TANZANIA
ALIYOYASEMA WAZIRI WA NISHATI, DKT MEDARD KALEMANI
Tunamshukuru Rais Yoweri Kaguta Museveni kwa kuamua kuchagua kukubaliana na Rais, Dkt. John Pombe Magufuli katika kupitisha bomba la mafuta ghafi katika ardhi ya Tanzania, jambo litakaloleta faida kwa nchi zote mbili.
Mawaziri wa Uganda na Tanzania, tunachofanya ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali mbili kwani baada ya kusaini mkataba wa makubaliano ya nchi hizi mbili, Mawaziri tuliainisha mambo ya msingi ya utekelezaji wa mradi na kulikuwa na masuala mengi ya kujadili lakini katika vikao mbalimbali vya ngazi ya Mawaziri tumeendelea kukubaliana katika masuala mbalimbali yatakayowezesha mradi kusonga mbele.
Suala la msingi ni kuwa, mradi ulishaanza kutekelezwa kwa kufanyika kazi za awali ikiwemo tathmini ya mazingira ambayo kwa upande wa Tanzania imekamilika na upatikanaji wa eneo kutapojengwa matenki matano yatakayohifadhi mafuta lita laki tano kila moja mkoani Tanga ambapo taratibu za ujenzi zinaendelea.
Mradi huu unatekelezwa hatua kwa hatua hivyo kuna kazi zinaendelea kutekelezwa wakati tunaendelea na majadiliano ikiwemo za utafiti wa kijiokemia, kijiolojia na kijiotekniko na kuna kazi zitakazofuata baada ya majadiliano.
Mara baada ya majadiliano haya ya leo zipo hatua zitakazofuata ambazo ni majadiliano kimkataba kati ya Serikali ya Tanzania na wawekezaji wa mradi ambao ni kampuni ya Total E&P ya Ufaransa, Tullow Oil ya Uingereza na CNOOC ya China na pia wenzetu watafanya majadiliano husika na wawekezaji hawa.
Kwa ujumla tumejipanga kuwa, majadiliano yote ya mradi na maandalizi ya mradi kati ya pande zote mbili yakamilike mwezi Juni mwaka huu ili ujenzi wa mradi pia uanze mwezi Juni na tunataka kukamilisha mradi huu ndani ya miezi 36 mara baada ya ujenzi kuanza.
ALIYOYASEMA WAZIRI WA NISHATI NA MAENDELEO YA MADINI WA UGANDA, IRENE MULONI
Mazungumzo ya leo kati ya pande hizi mbili yamefanyika vizuri na yale tuliyokubaliana, kila upande unaenda kuyawasilisha katika uongozi wa juu wa nchi kabla ya kuendelea na hatua nyingine za majadiliano.
Kwa ujumla kuna majadiliano mbalimbali yaliyo mbele yetu ikiwemo majadiliano ya ubia wa kampuni (shareholding agreement) ambayo tunatarajia yakamilike mwezi Juni ili kuweza kuanza ujenzi wa mradi.
Timu za Majadiliano ya Kitaifa kutoka Uganda na Tanzania (GNT) bado zina kazi kubwa ya kufanya na tunaamini wataendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha kuwa wananchi wa nchi hizi mbili wanafurahia mradi huu muhimu.

No comments