DC MBONEKO ASEMA ATAKAYEDOKOA FEDHA ZA SERIKALI ATAZITAPIKA
Mkuu
wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko (pichani) amewataka watendaji wa
serikali kutumia fedha zinazotolewa na serikali kwa malengo
yaliyokusudiwa kwa kuepuka tamaa vinginevyo watakao kwenda kinyume
watazitapika fedha hizo.
Mboneko
ametoa kauli hiyo Februari 16,2019 wakati Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa
Shinyanga (CCM) Mhe.Azza Hilal Hamad akitoa ufafanuzi kwa wananchi wa
kata ya Usule kuhusu shilingi milioni 146.6 zilizotolewa na serikali kwa
ajili ya ujenzi wa madarasa na nyumba za walimu katika shule ya msingi
Masunula iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Mkuu
huyo wa wilaya alisema serikali haitasita kuwachukulia hatua za
kisheria watu wote watakaobanika kutumia vibaya fedha za serikali.
“Msithubutu kudokoa fedha za serikali, hakuna pesa ya serikali
itapotea,ukidokoa utazitapika au tutakupeleka gerezani,fedha za serikali
zinapokuja zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa,mnaponunua vifaa vya
ujenzi nunueni kwa bei ya jumla na siyo reja reja”,alisema Mboneko.
Aidha aliwataka wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo kwani
serikali pekee haiwezi kufanya kila kitu huku akisisitiza kuwa kuna
maendeleo yanaletwa na serikali lakini mengine yanatokana na wananchi
wenyewe.
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga, Azza Hilal Hamad alisema
kupatikana shilingi milioni 146.6 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya
ujenzi wa nyumba mbili za walimu na madarasa mawili kunatokana na
jitihada kubwa aliyofanya kama mbunge kuipigania shule ya Msingi
Masunula ambayo imekuwa ikifanya vizuri katika matokeo ya darasa la
saba.
“Shule ya Msingi Masunula kwa miaka mitatu mfululizo 2016,2017 na
2018 imekuwa ikiongoza kwa shule za serikali kiwilaya na mkoa wa
Shinyanga katika matokeo ya darasa la saba…baada ya kulijua hilo, mimi
nilisikitika na ninasikitika sana kusikia kwamba pamoja na jitihada
kubwa za walimu wanazozifanya,eti walimu hapa shuleni hawana nyumba za
kuishi lakini hata vyoo tu hawana”,
“Hivi hawa walimu kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa watoto wetu sisi
tumeshindwa kujenga hata vyoo?,kweli ndugu zangu,kuna kitu gani
hapa,yaani kabisa tunasimama tunasema shule yetu inaongoza kimkoa kwa
ufaulu,kweli tuko sawa sawa kwa hili?”,alihoji Azza.
“Niliumia sana kuambiwa hakuna nyumba ya mwalimu hata
mmoja,matokeo yake walimu wengine wanakaa Didia,nikaamua kulibeba na
kwenda kulisemea kwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa alipopita
Tinde,nikaiomba serikali iangalie ya msingi Masunula na kwa sababu
serikali yetu ni sikivu baada ya kuomba fedha Julai 2018,serikali
imetuletea fedha shilingi milioni 146.6 mwezi Januari 2019”,alisema Azza.
Mh. Azza alieleza kuwa kati ya shule zote zilizopewa fedha,Masunula
ndiyo shule iliyopewa fedha nyingi kama motisha kwa sababu ya matokeo
mazuri na siyo vinginevyo.
“Sasa ni jukumu letu wananchi kuhakikisha kuwa fedha tulizopewa
twende tukajitolee,tukafanye nguvu kazi ili tuwe na uchungu,ni jukumu
letu sasa kwamba tumepewa fedha ya kujenga nyumba mbili sisi tujenge
tatu,kufanya kwenu vizuri itaonesha shukrani kwa serikali”,alisema.
“Nataka tuibadilishe
Masunula,tuibadilishe kata ya Usule,Masunula ifanane na yale matokeo
mazuri ya mtihani wa darasa la saba yanayosomeka kule, sasa siyo matokeo
mazuri halafu wazazi hamtaki kuwaunga mkono watoto wetu,kwa sababu kama
watoto wapo kwenye mazingira magumu,na walimu wanafundisha kwenye
mazingira magumu na mazingira ndiyo haya,tukiwaboreshea mazingira
matokeo yatakuwa mazuri zaidi,si mnaweza kusikia darasa la zima
limefaulu!”,aliongeza Azza.
ANGALIA PICHA
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akizungumza kwenye mkutano
wa hadhara katika kijiji cha Masunula kata ya Usule halmashauri ya
wilaya ya Shinyanga na kuwahimiza watendaji wa serikali na wananchi
kutumia fedha zinazotolewa na serikali kwa malengo yaliyokusudiwa.
Kushoto ni Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga, Azza Hilal Hamad
(CCM). Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akizungumza kwenye mkutano
wa hadhara katika kijiji cha Masunula kata ya Usule halmashauri ya
wilaya ya Shinyanga.
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga, Azza Hilal Hamad (CCM)
akiwasisitiza wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo badala ya
kusubiri serikali iwafanyie kila kitu.
Wananchi wakimsikiliza Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga, Azza Hilal Hamad (CCM).
Mwananchi akiuliza swali kwa viongozi waliofika katika kata hiyo.
Wananchi wakiwa katika eneo la mkutano.
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga, Azza Hilal Hamad (CCM)
akikabidhi bati moja ikiwa ni sehemu ya mabati 20 aliyotoa kwa ajili ya
ujenzi wa vyoo katika shule za msingi Masunula na Usule.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Andrew Mitumba akimshukuru mbunge Azza Hilal kwa kutoa mabati 20.
Mwenyekiti wa kijiji cha Masunula Kiyenze Majinge (kwenye nguo ya bluu)
akiwaongoza Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, Mbunge wa Viti
Maalum mkoa wa Shinyanga, Azza Hilal Hamad na viongozi mbalimbali kwenda
kuona eneo ambapo patajengwa nyumba za walimu pamoja na madarasa katika
shule ya msingi Masunula.
Mwalimu
mkuu wa shule ya msingi Masunula Gadius Kuyerwa ( wa nne kutoka kulia)
akionesha na kuelezea kuhusu eneo ambapo patajengwa nyumba za walimu.
Mkuu
wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko(wa pili kulia) na diwani wa kata
ya Usule, Amina Bundala wakioneshana eneo la ujenzi wa nyumba za
walimu.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
No comments