Kisa CAG Zitto, Ndugai uso kwa uso mahakamani leo
Kesi ya kikatiba kuhusu kinga ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad na mamlaka ya Bunge kuwahoji watu wanao tuhumiwa kulidhalilisha Bunge, leo Ijumaa Februari 15, 2019 inatarajiwa kusikilizwa.
Kesi hiyo ya kikatiba namba 1 ya 2019 imefunguliwa Mahakama Kuu masjala kuu na mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Inatarajiwa kusikilizwa na jopo la majaji watatu, litakaloongozwa na Jaji Firmin Matogolo, Jaji Benhajj Masoud na Jaji Elinaza Luvanda.
Katika kesi hiyo, Zitto ambaye pia ni Kiongozi wa ACT anaiomba Mahakama Kuu itoe tafsiri ya kinga ya CAG iliyopo kikatiba na pia kutoa tafsiri ya Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge katika kushtaki watu wanaosemekana kudharau Bunge.
Zitto alifungua kesi hiyo baada ya Ndugai kupitia kwenye vyombo vya habari na baadaye kumwandikia barua CAG akimtaka afike mbele ya kamati hiyo ya Bunge kuhojiwa kutoka na kauli yake aliyoitoa akiwa nchini Marekani kuwa Bunge la Tanzania ni dhaifu.
Profesa Assad alitoa kauli hiyo kama maoni yake akiwa New York Marekani, wakati akihojiwa na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Redio ya Umoja wa Mataifa, Anold Kayanda, kulingana namna ambayo taarifa zake za ukaguzi zinavyofanyiwa kazi.
Kufuatia wito huo wa Ndugai kwa CAG, Zitto anaiomba mahakama hiyo itamke na kuamuru kuwa Spika alishindwa kuzingatia wajibu wake wa kufuata Katiba katika amri ya kumtaka CAG kufika mbele ya kamati hiyo Januari 21, 2019.
Pia anaiomba mahakama itamke na kuamuru kwamba amri ya Ndugai kwa CAG ni kinyume cha Katiba kwa kukinzana na masharti ya Ibara za 26 (1), 18(a) (b) na (d) za Katiba ya Tanzania na kwamba wito huo ni batili.
Vilevile anaiomba mahakama hiyo zuio la kudumu kumzuia Ndugai, watumishi wake na au wakala wake kutokuchukua hatua yoyote ikiwemo kuamuru au kuelekeza mtu yeyote kumkamata na au kumchukua CAG kwenda Dodoma kuhojiwa na Kamati ya Bunge kuhusu kauli yake hiyo.
Hivyo wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, Zitto kupitia kwa wakili wake, Fatma Karume anatarajiwa kutoa hoja zake za kisheria kuishawishi mahakama kuwa CAG analindwa na kinga kwa mujibu wa Katiba.
Katika hoja zake hizo, Wakili Karume atakuwa na wajibu wa kuishawishi mahakama kuwa kwa kinga hiyo aliyo nayo CAG kikatiba, Spika au Bunge halina mamlaka ya kumhoji kwa lolote alilolifanya au kulitamka mahali popote, ikiwemo kauli hiyo aliyoitoa akiwa Marekani.
Upande wa wadaiwa pia kupitia kwa mawakili wake, jopo la mawakili wa Serikali, utakuwa na nafasi ya kupangua hoja za upande wa mdai (Zitto), huku ukitumia vifungu vya sheria na ibara za Katiba, kuishawishi mahakama kuwa kinga ya CAG si kamili bali ina mipaka.
Hata hivyo, CAG alishafika mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge na kuhojiwa kwa kauli hiyo na sasa anasubiri uamuzi wa Bunge kulingana na mapendekezo ya kamati hiyo.
No comments