Makundi ya muqawama Palestina: Msikiti wa Al Aqsa ni mstari mwekundu kwetu
Makundi ya muqawama na mapambano ya Palestina yametoa onyo kwa utawala ghasibu wa Kizayuni kutokana na kuendelea kuuvunjia heshima msikiti mtukufu wa Al Aqsa, kibla cha kwanza cha Waislamu.
Makundi ya muqawama ya Palestina yametoa taarifa maalumu leo na kusisitiza kuwa, msikiti wa Al Aqsa ni mstari mwekundu kwa makundi hayo na kubainisha kwamba, katu hayatounyamazia kimya uchokozi na uvamizi wa kila mara unaofanywa na askari wa utawala haramu wa Israel dhidi ya msikiti huo na kwamba utawala huo wa Kizayuni unaoikalia Quds kwa mabavu lazima uwajibike kwa jinai zake za kinyama unazotenda.
Makundi hayo ya muqawama yametoa mwito kwa Wapalestina yakisisitiza kwamba: Ili kuyalinda matukufu ya Kiislamu, kwanza kabisa ukiwa ni msikiti mtukufu wa Al Aqsa, wakusanyike kwenye msikiti huo na kufanya maandamano makubwa katika sehemu yake ya Babu-Rahmah.Waislamu wa Palestina wakisali Sala ya Ijumaa kwenye uwanja wa msikiti wa Al Aqsa
Katika taarifa yao hiyo, makundi ya muqawama ya Palestina yamesisitiza pia kwamba: Uchokozi na uvamizi huo wa utawala haramu wa Kizayuni unafanyika mbele ya kimya cha kuaibisha cha nchi za Kiarabu na Kiislamu na ushindani wa wazi wazi wa baadhi ya watawala wa nchi za Kiarabu wa kugombania kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Hali katika msikiti wa Al Aqsa imekuwa tete na ya taharuki kufuatia hatua ya hivi karibuni ya utawala wa Kizayuni ya Israel kuwafungia Waislamu Wapalestina Babu-Rahmah, moja ya milango ya kuingilia msikiti huo mtukufu.
Wakati huo huo Ismail Haniya, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS ametoa taarifa, akiwataka wananchi wa Palestina waishio Baitul Muqaddas, Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan na ardhi nyingine zinazokaliwa kwa mabavu wafanye maandamano makubwa kesho Ijumaa kuelekea msikiti wa Al Aqsa kwa lengo la kukihami kibla hicho cha kwanza cha Waislamu.../
No comments