Waziri Ummy awatoa hofu wananchi kuhusu chanjo ya Saratani ya mlango wa kizazi
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amewatoa hofu Wananchi kwa kusisitiza kuwa chanjo ya kuwakinga wasichana na Saratani ya Mlango wa kizazi haihusiani na uzazi wa mpango wala kumzuia msichana kuja kupata uja uzito baadae.
Ameyasema hayo leo wakati akiongea na Waandishi wa Habari katika siku ya Saratani Duniani, iliyofanyika katika Ukumbi wa Idara ya Habari Bunge jijini Dodoma, huku kauli mbiu ya mwaka huu ikiwa ni "NITAFANYA JITIHADA ZOTE KUPUNGUZA JANGA LA SARATANI DUNIANI".
Waziri Ummy amesema kuwa Chanjo ya Mlango wa kizazi ni salama na imethibitishwa na Shirima la Afya Duniani kwaajili yakuwakinga Wasichana dhidi ya maambulizi ya Saratani ya Mlango wa kizazi. " Chanjo ya kuwakinga wasichana na saratani ya mlango wa kizazi haihusiani na uzazi wa mpango, ni chanjo ambayo imethibitishwa na Shirika la Afya Duniani kwaajili yakuwakinga wasichana dhidi ya maambukizi ya Saratani ya mlango wa Kizazi" Alisema Waziri Ummy
Waziri Ummy amesema kuwa katika kila wagonjwa wa Saratani 100, takribani wagonjwa 31 ni wanawake wa Saratani ya Mlango wa kizazi, hivyo amewahasa wazazi na walezi nchini kuhakikisha wasichana wanaostahili kupata chanjo hii, wanaipata bila vikwazo vyovyote ili kutokomeza kabisa Saratani hii nchini. "Katika kila wagonjwa wa Saratani 100, Wagonjwa takribani 31 ni wanawake wa Saratani hii ya Mlango wa kizazi, kwahiyo hatuna haja ya kuiogopa chanjo hii kwasababu ndio itayowakinga watoto wetu na maambukizi ya Saratani ya mlango wa kizazi" alisema Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Tafiti za Saratani (IARC), zinaonyesha kwamba kwa Tanzania kunatokea mgonjwa 1 wa Saratani kwa kila watu 1000, hivyo Tanzania inakua na wagonjwa wapya wa Saratani 55,000 kwa mwaka na takribani wagonjwa 28,610 hufariki kwa mwaka, ambapo ni vifo asilimia 52 ya wagonjwa wapya.


No comments