Breaking News

Dkt. Gwajima ataka mabadiliko ya kiutendaji kwa watoa huduma za afya nchini



Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Dorothy Gwajima ameziagiza kamati za huduma za afya Mkoa (RHMT) na Wilaya(CHMT) kuhakikisha wanasimamia kwa weledi huduma zinazotolewa katika vituo vya afya nchini.

Ameyasema hayo alipokuwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua utendaji kazi wa vituo vya afya vya Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Jijini Dodoma.

Dkt.Gwajima amesema kuwa ni kazi ya Kamati za kutoa huduma za afya nchini kuhakikisha wanasimamia kwa umakini mkubwa huduma ambazo zinapaswa kutolewa kwa wananachi.

“Serikali imejenga miundombinu ya afya nchini kwa sasa lakini wananchi wanachohitaji ni uhakika wa huduma bora za afya ambazo zinakidhi mahitaji yao hivyo ni vyema kamati hizo zikahakikisha huduma zinaboreshwa katika vituo vyote vya afya nchini” Amesema Dkt. Gwajima

Dkt Gwajima anaendelea kufafanua kuwa watoa huduma za afya wote nchini wanatakiwa kutumia taaluma walizonazo katika kuwahudumia wananchi ili kupunguza malalamiko yanayotolewa katika Sekta ya afya

“Watoa huduma za afya nchini wanapaswa kuhakikisha wanakuwa wazalendo, kuwa na huruma na wagonjwa ili kujenga imani kwa wananchi kuwa huduma za afya zimeboreshwa”Anafafanua Dkt. Gwajima.

Ameendelea kusema kuwa kuwepo kwa miundombinu ni jambo la muhimu sana lakini ifike mahali ambapo sekta ya afya ijitathmini kwa kina kama kweli inatoa huduma stahiki kwa jamii hasa katika utendaji kazi, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha anatumia weledi katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Amesema kuwa miundombinu ya vituo vya afya nchini imeboreshwa kwa kiwango kikubwa kinachohitajika ni mabadiliko katika utendaji kazi hasa katika utoaji wa huduma kwa jamii ili vituo vya Serikali visiwe magofu.

“Ili kuongeza idadi ya wateja katika vituo vya afya nchini lazima kuwepo na ukarimu ,lugha nzuri kwa mteja ,uwajibikaji bila kusahau uzalendo ambavyo hivi vyote vitaleta chachu katika matokeo bora kwenye utoaji huduma za afya kwa jamii” Ameongezea Dkt.Gwajima

Dkt.Gwajima ameviagiza vituo vyote vya afya nchini kuhakikisha wanakuwa ma mpango kazi ambao utawaongoza na kuwawezesha kufanya tathmini ya kilichofanyika kutafutiwa ufumbuzi ili kufikia malengo waliojiwekea kama kituo.

Aidha amewaagiza kudumisha mahusiano mazuri baina ya watumishi katika ngazi ya Zahanati, Kituo cha afya, Halmashauri, Mkoa na Wizarani kwa kuwa kwa mabadiliko yakifanyika kutaongeza uwajibikaji na utoaji wa huduma bora utaongezeka.

Pata habari motomoto na za uhakika kila siku kila zinapojiri katika nyanja mbalimbali ikiwemo Siasa, Michezo, Ajira, uchumi, Mapenzi, Udaku/Umbea n.k .Kwa kudownload APP hii Bofya HAPA Kudownload.

BOFYA HAPA

No comments