Mbowe na Esther Matiko Waachiwa Kwa Dhamana
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo imetengua uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wa kuwafutia dhamana Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini wa chama hicho, Ester Matiko, kwa kukubali maombi yao ya dhamana ikiwa ni pamoja na kuripoti mahakamani mara moja kwa mwezi badala ya polisi kila wiki.
Wakati wa hukumu hiyo iliyotolewa na Jaji Sam Rumanyika, ulinzi mahakamani hapo ulikuwa umeimarishwa kwa askari wengi waliotanda sehemu mbalimbali.
“Hii ni rufaa mojawapo ambayo sijawahi kuiona katika kazi yangu ya ujaji. Maofisa wa mahakama kama mahakimu wanapaswa kutumia utashi wao kuamua haki za watu kwa kuzingatia haki maana ni hatari sana kumnyima dhamana mtu bila sababu za msingi,” alisema Jaji Rumanyika wakati wa kutoa hukumu hiyo na kuongeza:
“Kuanzia sasa, naagiza Mbowe na Matiko waachiwe huru mara moja na watatakiwa kuripoti mahakamani mara moja kwa mwezi badala ya polisi kila wiki.”
Novemba 23, 2018 Jaji Wilbard Mashauri akiwa Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, alifuta dhamana ya Mbowe na Matiko kutokana na kukiuka masharti ya dhamana.
Wawili hao walikata rufaa katika Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga uamuzi wa Mahakama ya Kisutu kufuta dhamana yao ambapo rufani yao ilipangwa kusikilizwa na Jaji Rumanyika.
Hata hivyo, baada ya Mahakama Kuu chini ya Jaji Rumanyika kusikiliza mapingamizi ya pande zote, iliamua kuanza usikilizaji wa rufaa hiyo.
Upande wa serikali ukiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Paul Kadushi, ulidai kuwa wamekata rufaa katika Mahakama ya Rufani kupinga maamuzi yaliyotolewa na Mahakama Kuu.
Hata hivyo, Machi 1 mwaka huu, Mahakama ya Rufaa chini ya jopo la majaji watatu: Stella Mugasha, Dk Gerald Ndika na Mwanaisha Kwariko, ilitupilia mbali pingamizi hilo la serikali na kuamuru kesi hiyo irudishwe Mahakama Kuu kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa.

No comments