Breaking News

WABUNGE LIJUALIKALI, KIWANGA WAACHIWA KWA DHAMANA



Mbunge wa Mlimba, Suzan Kiwanga.

WABUNGE wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Suzan Kiwanga (Mlimba), Peter Lijualikali (Kilombero) na wanachama wenzao saba, leo wamepata dhamana baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro kutupilia mbali maombi ya upande wa mashtaka ya kupinga dhamana yao.



Wabunge hao pamoja na wenzao, wamepata dhamana baada ya kusota rumande kwa takriban wiki mbili tangu walipofikishwa mahakamani hapo.



Watu hao wamepewa dhamana baada ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo, Elizabert Nyembele, anayesikiliza kesi hiyo kupitia hoja za upande wa mashtaka za kupinga dhamana na zile za upande wa utetezi zilizoeleza upungufu ya maombi hayo.



Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali.

Hata hivyo, Nyembele amesema lazima washtakiwa hao wakidhi masharti ya dhamana kwa kila mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja atakayewasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani si chini ya Sh. milioni tano na atakayeweza kutoa dhamana ya Sh. 3,756,000.


Baada ya kupewa dhamana washtakiwa hao walijikuta kwenye wakati mgumu kutokana na wadhamini waliojiandaa kutokuwa na hati ya mali zisizohamishika.


Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) Devota Minja ambaye amefika mahakamani akiwa na wafuasi wengine wa chama hicho alionekana kuhangaika ili kupata wadhamini wenye sifa huku akiwahakikishia washtakiwa hao kuwa watadhaminiwa kabla ya mahakama kufungwa.


Watu hao wanashtakiwa kwa kesi ya jinai namba 43 ya mwaka 2019 na kwamba Novemba 26, 2017 walitenda makosa manane likiwamo la kuharibu mali na kuchoma ofisi ya serikali ya kijiji cha Sofi wilaya ya Malinyi.


Awali, upande wa mashtaka ukiwakilishwa na wakili wa serikali mwandamizi Neema Haule, uliwasilisha maombi ya kupinga dhamana kwa madai taratibu za kisheria za kupinga dhamana ya washtakiwa hao zimefuatwa na wametumia kifungu cha sheria namba 392 A cha mwenendo wa makosa ya jinai.



Naye wakili upande wa utetezi, Hekima Mwasipu, aliwasilisha hoja za kupinga zuio hilo la dhamana akidai kuwa halikufuata taratibu za kisheria hivyo si halali.

No comments