Breaking News

Serikali Yapiga Marufuku Kutangaza Magonjwa ya Mifugo

Serikali imeogesha mifugo milioni 32, sawa na asilimia 56 ya mifugo milioni 57 iliyopo nchini, katika kipindi cha miezi mitatu, tangu kuzinduliwa kwa kampeni ya kitaifa ya uogeshaji mifugo.


Pia, imepiga marufuku mtu yeyote kutangaza kuwepo magonjwa ya mifugo, isipokuwa yule aliyepewa mamlaka hayo kwa mujibu wa Sheria.


Hayo yamesemwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, wakati akizungumzia tathmini ya kampeni ya uogeshaji kitaifa, iliyofanyika kwenye josho la kwanza kujengwa na Wajerumani katika nchi za Afrika Mashariki liitwalo Nunge, lililojengwa mwaka 1905 wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.


Alisema Sheria za Kimataifa na Sheria ya Magonjwa ya Mifugo Namba 17 ya mwaka 2003, inazuia kufanya hivyo.


Mpina alisema shabaha ya kuzuiwa kufanya hivyo kwa sababu baadhi ya watu wanaweza kujitokeza kupeleka hofu kwa wananchi na kusababisha kuharibu biashara hiyo.


Hivyo, alisema Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo (DVS) ndiye aliyepewa dhamana ya kutangaza ugonjwa wowote wa mifugo kwa niaba ya Watanzania na wala sio mtendaji yeyote yule wa serikali.


“Ndugu zangu vyombo vya habari msije mkaingia kwenye mgogoro wa serikali, mambo ya chakula ni sensitive (nyeti) tukifanya hivyo tutakuwa tunapeleka maneno ya taharuki kwa wananchi, tumuachie aliyepewa jukumu hilo, hivyo sitegemei tena kama watu wengine wataendelea kufanya hivyo,” alisema Mpina.


Alisema nchi imejipanga vizuri kudhibiti magonjwa ya mifugo na ndio maana inazo kanda nane za uchunguzi wa magonjwa ya mifugo, hivyo Watanzania wako salama Tanzania iko huru na magonjwa.


Alisema kwa sasa Tanzania inazalisha chanjo nane na kufikia Septemba hadi mwakani, kutakuwa na chanjo 11 ili mifugo ichanjwe isipatwe tena na magonjwa.


Mpina alisema ifikapo Julai mosi mwaka huu wizara yake itakuwa imeshatoa kanuni za namna ya uendeshaji wa kazi ya uogeshaji ili kila mmoja afahamu wajibu wake.


Alisisitiza agizo lake la ukarabati wa majosho na ifikapo Julai Mosi mwaka huu, halmashauri ambayo itakuwa haijakarabati majosho, itazuiliwa kukusanya mapato huku akizindikia barua za kusudio la kuzizuia kukusanya mapato halmashauri hizo.


Majosho 132 kati ya majosho mabovu 1,124 yameshakarabatiwa. Hivyo, asilimia 11 ya agizo hilo limetekelezwa, ikiwa ni miezi mitatu tangu limetolewa.


Aliupongeza Mkoa wa Kagera kwa kukarabati majosho 34, Mkoa wa Mwanza wamekarabati majosho 19, Mkoa wa Arusha majosho 11, Mkoa wa Dodoma majosho mawili tu na wengine hawajafanya hivyo.


Mpina alisema halmashauri zote nchini zinakusanya zaidi ya Sh bilioni 30 kwa mwaka kutokana na sekta ya mifugo, lakini halmashauri zinatenga fedha kidogo za kusaidia mifugo.

Pata habari motomoto na za uhakika kila siku kila zinapojiri katika nyanja mbalimbali ikiwemo Siasa, Michezo, Ajira, uchumi, Mapenzi, Udaku/Umbea n.k .Kwa kudownload APP hii Bofya HAPA Kudownload.BOFYA HAPA

No comments