Simba yafanya kufuru Algeria
UKISIKIA jeuri ya fedha ndio hii kwani Simba wamefanya mambo makubwa kwenye ardhi ya Jiji la Bechar, Algeria wakisubiri kuvaana na wenyeji, JS Saoura katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa kesho Uwanja wa Agosti 20, 1955.
Simba imetua juzi Jumatano jijini humo na kupokewa kishujaa, huku Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania ukisimamia shoo nzima kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri.
Mara baada ya kutua mjini Algeria, jeshi la Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, halikutaka mzaha na moja kwa moja kuanza mazoezi ya kujiandaa na mchezo huo kwenye Uwanja wa Hoteli ya New Day ilipofikia timu hiyo.
Simba imefikia katika hoteli hiyo ya nyota nne yenye vyumba 226, ambapo kuna bwawa la kuogelea, ‘gym’ ya kufanyia mazoezi, chumba cha ‘massage’, mgahawa wa kisasa na ukumbi wa mikutano.
Gharama ya chini ya chumba chenye uwezo wa kuchukua zaidi ya watu wawili ni dola 127 (sawa na Sh 286,313) ambapo mpaka itakaporejea timu hiyo itakuwa imetumia Sh milioni 16 kwa ajili ya malazi pekee.
Mbali na gharama hiyo ya malazi, Wekundu hao wa Msimbazi wanatarajia kutumia zaidi ya Sh milioni 10 kwa ajili ya chakula kwa siku nne watakazokaa nchini Algeria.
Pia Wekundu hao wa Msimbazi wametumia zaidi ya Sh milioni 80 kuwalipia wachezaji tiketi za ndege kama nauli ya kwenda na kurudi.
Akizungumzia mchezo huo Mwenyekiti wa Simba, Swedy Mkwabi, alisema wamefurahishwa na jinsi walivyopata mapokezi na kuahidi ushindi siku ya kesho.
“Tupo sehemu salama, mazingira ya hoteli ni mazuri, wachezaji washindwe wenyewe kesho,” alisema Mkwabi.
Simba inashika nafasi ya pili kwenye Kundi D, huku Al Ahly ya Misri ambayo wikiendi hii itakuwa mgeni wa AS Vita, mjini Kinshasa, ndiyo inaongoza ikiwa na pointi saba.
No comments