Ndayiragije kumrithi Pluijm Azam FC
BAADA ya Hans van der Pluijm, kung’olewa kwenye benchi la ufundi la Azam FC, kuna asilimia kubwa ya Kocha wa KMC, Etienne Ndayiragije, kubebeshwa jukumu la kukinoa kikosi hicho.
Hivi karibuni Azam walimwondoa kocha wao, Pluijm, kutokana na mwenendo wa timu kutokuwa mzuri kwenye baadhi ya michezo yake na timu kukabidhiwa kwa aliyekuwa mwalimu msaidizi wa timu hiyo msimu uliopita, Iddy Cheche.
Chanzo cha habari za kuaminika kutoka ndani ya klabu hiyo kililiambia BINGWA juzi kuwa Azam wanamhitaji Ndayiragije na wameshafanya naye mazungumzo, mambo yakikaa sawa ataanza kukinoa kikosi hicho.
“Kuna mambo madogo tu ya mikataba ambayo yanakwamisha mwalimu kuanza kazi, wakishayakamilisha ndiye atakuwa kocha mpya wa Azam,” alisema.
Awali Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Abdulkarim Amin ‘Poppat’, aliliambia BINGWA kuwa ni makocha wengi ambao wametuma maombi lakini hawajaridhika nao.
“Tutamtangaza atakayemrithi Pluijm muda ukifika, tunalifanyia kazi hili hivi karibuni mtajua,” alisema.
No comments