Taarifa kuhusu kuanza kwa vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge Jijini Dodoma tarehe 11 hadi 31 Machi, 2019.

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
BUNGE LA TANZANIA
Simu: +255 026 23222761-5
Fax No. +255 026 2322624
E-mail: info@bunge.go.tz
Ofisi ya Bunge,
S.L.P. 941,
DODOMA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU KUANZA KWA
VIKAO VYA KAMATI ZA BUNGE TAREHE 11 HADI 31
MACHI, 2019, MJINI DODOMA
_________
1.0 UTANGULIZI
Kamati za Kudumu za Bunge zitaanza kukutana Jumatatu tarehe 11
hadi 31 Machi, 2019 Mjini Dodoma kutekeleza majukumu ya
kibunge kabla ya Mkutano wa Kumi na Tano wa Bunge
uliopangwa kuanza tarehe 02 Aprili, 2019. Kwa mujibu wa Ratiba
ya Shughuli za Kamati, Waheshimiwa Wabunge wote wanapaswa
kuwasili Mjini Dodoma Jumapili tarehe 10 Machi, 2019 tayari kwa
ajili ya kuanza kwa vikao vya Kamati.
Shughuli zitakazotekelezwa na Kamati hizo ni pamoja na:
a) KUPOKEA WASILISHO LA SERIKALI KUHUSU KIWANGO CHA
UKOMO WA BAJETI
Katika kipindi hicho cha vikao vya Kamati za Bunge, siku ya
tarehe 12 Machi 2019, Wabunge watapokea Wasilisho la
Mapendekezo ya Serikali kuhusu Mpango na Kiwango cha Ukomo wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 kwa mujibu
wa Kanuni ya 97 ya Kanuni za Bunge Toleo la Januari, 2016.
b) KUFANYA ZIARA ZA UKAGUZI WA MIRADI
Kamati zitafanya ziara za ukaguzi wa miradi ya Maendeleo
iliyotengewa fedha katika Bajeti ya mwaka 2018/2019 kwa
mujibu wa Kanuni ya 98(1) ya Kanuni za Bunge Toleo la
Januari, 2016. Kamati zitakagua miradi ya uwekezaji
liyotekelezwa na Serikali kupitia Mashirika ya Umma. Aidha,
Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Hesabu za
Serikali za Mitaa (LAAC) zitafanya ziara za ukaguzi wa miradi
mingine iliyotekelezwa na Serikali ili kulinganisha matokeo ya
utekelezaji na thamani halisi ya fedha za Umma zilizotumika
katika miradi hiyo.
c) KUFANYA UCHAMBUZI WA BAJETI
Katika vikao hivyo pia Kamati zitafanya uchambuzi wa Taarifa
za Utekelezaji wa Bajeti za Wizara inazozisimamia kwa Mwaka
wa Fedha unaoishia 2018/2019 kwa ajili ya kufanya ulinganisho
kuhusu makadirio ya matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa
Fedha 2019/2020 kwa mujibu wa Kanuni ya 98(2) ya Kanuni za
Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016.
d) KUFANYA UCHAMBUZI WA TAARIFA ZA UWEKEZAJI
Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) itafanya
uchambuzi wa Taarifa za Uwekezaji uliofanywa na Serikali
kupitia Mashirika ya Umma kwa mujibu wa Kifungu cha 12
cha Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Bunge Toleo la Januari,
2016.
e) UCHAMBUZI WA SHERIA NDOGO
Kamati ya Sheria Ndogo itafanya uchambuzi wa Sheria
Ndogo zilizowasilishwa wakati wa Mkutano wa Kumi na Nne
Bunge kwa mujibu wa Kifungu cha 11 cha Nyongeza ya Nane
ya Kanuni za Bunge Toleo la Januari, 2016
Ratiba zote za Shughuli za Kamati za Bunge ikiwa ni pamoja na
maeneo ambayo Kamati hizo zitafanya ziara zinapatikana katika
Tovuti ya Bunge ambayo ni www.parliament.go.tz. mara baada ya
Kamati hizo kuanza kazi.
Imetolewa na: Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa.
Ofisi ya Bunge
DODOMA
05 Machi, 2019
No comments