Uchaguzi, matumizi kugharimu tril. 21/-
SERIKALI imesema inatarajia kukusanya na kutumia Sh. trilioni 33.1 katika mwaka ujao wa fedha, huku Sh. trilioni 20.85 zikitengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na kugharamia uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.
Akiwasilisha mapendekezo ya serikali kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Taifa na kiwango na ukomo wa bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2019/20 kwa wabunge jijini Dodoma jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema sura ya bajeti ya mwaka huo wa fedha inaonyesha kiasi hicho kinatarajiwa kukusanywa na kutumika.
Dk. Mpango alisema Sh. trilioni 33.105 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika. Kati yake, mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Sh. trilioni 23.045.
Alisema mikopo ya ndani inakadiriwa kuwa Sh. trilioni 4.96, mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara Sh. trilioni 2.316 wakati misaada na mikopo yenye masharti nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo inatarajiwa kuwa Sh. trilioni 2.784.
"Kati ya Sh. bilioni 33,105.4 za matumizi ya kawaida na maendeleo, Sh. bilioni 20,856.8 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, matumizi haya yanajumuisha gharama za uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na maandalizi ya uchaguzi mkuu mwaka 2020," Dk. Mpango alisema.
Alibainisha kuwa matumizi ya maendeleo yanatarajiwa kuwa Sh. bilioni 12,248.6. Kati yake, Sh. bilioni 9,737.7 ni fedha za ndani na Sh. bilioni 2,510.9 ni fedha za nje.
"Mpango na bajeti ya mwaka 2019/20, unazingatia azima ya serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi thabiti wa Rais John Magufuli. Serikali itaendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kudhibiti mianya ya ukwepaji wa kodi," alisema.
Vilevile, waziri huyo alisema serikali itaendelea kuweka mkazo katika uwekezaji wa miundombinu ya umma na uboreshaji wa huduma za kijamii kwa lengo la kuleta maendeleo ya haraka.
"Napenda kuwahimiza Watanzania tuwajibike kulipa kodi na kuhakikisha tunatoa na kudai risiti kulingana na muamala uliofanyika," alisema.
Dk. Mpango alisema serikali itaendeleza mapambano dhidi ya rushwa, kuimarisha ulinzi wa rasilimali za umma na kudhibiti matumizi ya fedha za umma.
"Serikali pia itaongeza msukumo katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kutekeleza mpango wa kuboresha mfumo wa udhibiti wa biashara na uwekezaji," alisema.
VIPAUMBELE VITANO
Waziri huyo alisema mapendekezo hayo yanatekeleza vipaumbele vilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2016/17-2020/21.
Alivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda, akieleza kuwa miradi itakayotekelezwa katika eneo hilo ni ile yenye lengo la kujenga viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini hususan kilimo, madini na gesi asilia.
"Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi asilia, uanzishwaji na uendelezaji wa kanda maalum za kiuchumi na kongane za viwanda, viwanda vya kuongeza thamani mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, kuongeza thamani ya madini na usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu," alisema.
Dk. Mpango alisema kipaumbele kingine ni kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu, akibainisha miradi itakayotekelezwa katika eneo hilo kuwa ni ile yenye lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, elimu na ujuzi, upatikanaji wa chakula na lishe bora na huduma za majisafi na salama.
"Shughuli zitakazotiliwa mkazo ni pamoja na kugharamia utoaji wa elimu msingi bila ada, kupunguza vifo vya kinamama vinavyotokana na uzazi, utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Elimu, ujenzi na ukarabati wa vyuo vya ufundi stadi nchini na kuboresha huduma za maji vijijini," alisema.
Waziri huyo alisema kipaumbele kingine ni uboreshaji wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji, akieleza kuwa miradi itakayotekelezwa katika eneo hilo ni ujenzi na ukarabati wa miundombinu ambayo ni reli, bandari, nishati, viwanja vya ndege na barabara.
"Miradi hiyo ni pamoja na mradi wa kufua umeme wa maji Rufiji MW 2,115, kuboresha Shirika la Ndege Tanzania, ujenzi wa reli ya kati na kuendelea na utekelezaji wa mpango wa kuboresha mfumo wa udhibiti wa biashara na uwekezaji," alisema.
Alisema mpango huo pia umeweka msukumo katika kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuwekeza ikiwamo kupitia upya mfumo wa kitaasisi, kisera na kisheria pamoja na kanuni zake ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi katika kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo.
Dk. Mpango alisema kipaumbele cha tano ni kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa mpango, akieleza kuwa miradi itakayotekelezwa inalenga kuimarisha mifumo na taasisi za utekelezaji wa mpango, kuweka mfumo utakaowezesha upatikanaji wa uhakika wa rasilimali fedha na kuweka vigezo vya upimaji wa mafanikio ya utekelezaji.
Pata habari motomoto na za uhakika kila siku kila zinapojiri katika nyanja mbalimbali ikiwemo Siasa, Michezo, Ajira, uchumi, Mapenzi, Udaku/Umbea n.k .Kwa kudownload APP hii Bofya HAPA Kudownload. BOFYA HAPA
No comments