Wananchi watakiwa kushiriki Ujenzi wa Hospitali za Wilaya.
Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, katika kijiji cha Mlowa Barabarani wametakiwa kutoa ushirikikiano katika ujenzi wa Hospitali ya Wilaya hiyo ili kuleta maendeleo na kupunguza changamoto za afya nchini.
Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu Afya kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Dkt.Dorothy Gwajima wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua utendaji kazi wa vituo vya afya vya Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Jijini Dodoma.
Dkt. Gwajima amesema kuwa Serikali pekee haiwezi kufanikiwa katika kuleta maendeleo bila kuwepo ushirikiano kutoka kwa wananchi wake hivyo ni vyema wananchi wakashirikishwa kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
Amesema Serikali imejenga miundombinu ya afya nchini ikiwa na lengo la kuhakikisha huduma za afya zinaboreka kuanzia ngazi ya Zahanati, Vituo vya afya, Hospitali za Mikoa ili kupunguza changamoto katika sekta ya afya.
Akiendelea kufafanua amesema kuwa wananchi wanatakiwa kuwa na dhamira ya dhati ya kusimamia miradi ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya ili zijengwe kwa ubora kulingana na fedha zilizotolewa na Serikali.
“Wananchi hakikisheni mnasiamia ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Chamwino kwa umakini mkubwa kwa kuangalia gharama zinazotumika zinaenda sambamba na majengo yanayojengwa kwa kuwa Hospitali hizi ni mali ya wananchi” Amesisistiza Gwajima
Akifafanua kuhusu ubora wa huduma zinazotolewa kwenye vituo vya afya amesema Serikali imejenga miudombinu ya afya nchini lakini bado changamoto kubwa ni watendaji waliopo katika vituo hivyo kutotimiza majukumu yao kwa uadilifu katika kutoa huduma bora kwa jamii hali ambayo inasababisha wananchi wengi kutokufika katika vituo hivyo.
“ Baadhi ya watoa huduma wamekuwa na lugha chafu kwa wateja, kutokuwa na ukarimu, kutowajibika kikamilifu, uzembe, rushwa ambapo vitu vyote hivi vinapelekea wananchi kutokuja kutibiwa kwenye vituo vya afya vya Serikali na kukimbilia vituo binafsi, naagiza watoa huduma wote nchini kuhakikisha wanafanyakazi kwa weledi katika kuwahudumia wananchi” Amesema Gwajima
Aidha amewataka wananchi kuhakikisha wanatoa taarifa pale wanapojibiwa vibaya na watoa huduma za afya nchini na Serikali haitasita kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wote watakaobainika kuwa na makosa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chamwino, Athuman Masasi amesema kuwa watahakikisha wanakamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya hiyo kwa wakati ili wananchi waanze kupata huduma.
Pata habari motomoto na za uhakika kila siku kila zinapojiri katika nyanja mbalimbali ikiwemo Siasa, Michezo, Ajira, uchumi, Mapenzi, Udaku/Umbea n.k .Kwa kudownload APP hii Bofya HAPA Kudownload.
BOFYA HAPA
No comments