Malkia wa Meno ya Tembo' jela miaka 17
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemhukumu raia wa China, Yang Feng Glan (66) 'Malkia wa Meno ya Tembo’ na wenzake kifungo cha miaka 17 jela baada ya kukutwa na hatia ya kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh bilioni 13.9.
Washitakiwa wengine ni Salvius Matembo na Philemon Manase. Malkia wa Meno ya Tembo na wenzake wametakiwa kulipa faini ya Sh bilioni 27.
Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi pia amesema, nyumba iliyopo Muheza mkoani Tanga itataifishwa kwa kuwa ilihusishwa katika uhalifu huo.
Awali Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam iliwatia washitakiwa hao kwa kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh bilioni 13.
Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi amesema ni dhahiri kuwa washitakiwa hao walikuwa wakifahamiana kwa muda mrefu na walikuwa wakikusanya nyara hizo toka sehemu mbalimbali za nchi na kumpatia Malkia huyo.
Glan na wenzake walitetewa na mawakili Nehemia Nkoko na Hassan Kiangio.
Upande wa mashitaka katika kesi hiyo uliwasilisha mahakamani hapo mashahidi 11 kwa ajili ya kuthibitisha mashitaka hayo na baadaye, mahakama iliwakuta na kesi ya kujibu washitakiwa hao.
Ilidaiwa kuwa, Januari Mosi, 2000 na Mei 22, 2014 washitakiwa walijihusisha na biashara ya nyara za serikali.
Wanadaiwa kufanya biashara ya vipande 706 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilogramu 1889 zenye thamani ya Sh bilioni 13 bila ya kuwa na leseni iliyotolewa na Mkurugenzi Wanyama Pori.
Wanadaiwa kati ya Januari Mosi, 2000 na Mei 22,2014 Glan aliongoza na kufadhili vitendo vya kijinai kwa kukusanya na kusafirisha vipande hivyo bila kibali kutoka Mkurugenzi Wanyama Pori.
Washitakiwa Salvius na Manase wanadaiwa kuongoza makosa ya uhujumu uchumi kwa kusaidia biashara ya nyara za serikali kwa kukusanya, kusafirisha na kuuza meno ya tembo kwa nia yakujipatia faida.
Ilidaiwa mahakamani kuwa, Mei 21, 2014 Sinza Palestina wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, Manase alitoroka chini ya ulinzi wa Polisi D 7847 Koplo Beatus aliyekuwa akimshikilia kwa makosa ya kuhusika na biashara hiyo
No comments