Matola ajivunia rekodi kwa Simba, "tutawanyosha"

Leo ni siku ambayo Lipuli FC imejipambanua kuwa itawanyoosha mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania Bara Simba katika uwanja wake wa nyumbani wa Samora.
Hayo yameelezwa na kocha wa Lipuli FC, Seleman Matola kuelekea mchezo huo, ambapo amesema kuwa ana hamu ya kuwa wa kwanza kuwanyoosha wapinzani wake Simba ili kuwatibulia furaha waliyonayo hivi sasa kutokana na ushindi wanaoupata katika mechi zao.
"Unajua wapinzani wetu wapo vizuri ukizingatia matokeo yao yamekuwa chanya kwenye mechi zao, sasa hapo ndipo tunapataka tutibue furaha yao tuwe wa kwanza kubeba pointi tatu hapa nyumbani, madhaifu yao tunayajua tutawanyoosha mapema tu," amesema Matola.
Kwa mujibu wa takwimu, Simba wamekuwa wakipata taabu sana kuifunga Lipuli FC tangu klabu hiyo ya mjini Iringa ilipopanda ligi msimu wa mwaka 2017/18, ambapo leo wanakutana mara ya nne huku mechi zao zote zikiisha kwa sare.
Katika mchezo wa kwanza walipokutana mjini Iringa, timu hizo zilitoka sare ya kufungana bao 1-1 na mchezo wa marudiano katika Uwanja wa Taifa, walifungana bao 1-1 na mchezo wa kwanza msimu huu katika Uwanja wa Taifa, timu hizo zilitoka suluhu ya bila kufungana.
No comments