Mbunge Tundu Lissu amvaa Prof. Kabudi
MBUNGE wa Singida Mashariki (CHADEMA) na Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya upinzani bungeni, Tundu Lissu, “amempasha,” Prof. Palamagamba Kabudi.
Lissu anasema, waziri huyo mpya wa mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa, anapaswa kufahamu kuwa huu siyo tena watu wa kufokewa; na au kutishiwa kama watoto wa shule.
Anasema, “nimemsikia waziri wetu mpya wa Mambo ya Nje, akifokea na kutishia watu anaodai wanaisema vibaya na ‘kuibagaza’ nchi yetu. Kwa mujibu wa Katiba yetu, kuna tofauti kubwa kati ya Nchi na Serikali.”
Mwanasiasa huyo wa upinzani alikuwa akijibu kauli iliyotolewa na Prof. Kabudi, Ikulu jijini Dar es Salaam, mara baada ya kuapishwa kushika nafasi hiyo ya uwaziri wa mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa.
Akizungumza mbele ya rais, Prof. Kabudi alisema, “nchi hii iliyojengwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, siyo nchi ya kuchezewa. Siyo nchi ya kubezwa. Siyo nchi ya kudharauliwa. Siyo nchi kudhihakiwa.”
Akiongea kwa ujasiri
Amedai kuwa “…huu siyo wakati wa kuisema vibaya nchi yetu” na kuongeza, “hii sio nchi ya kuchezewa, na kwamba yeyote Mtanzania mwenye matatizo na nchi hii, ni vema akae kimya kama yamemshinda kusema ndani ya nchi yake.”
Prof. Kabudi na Dk. Mahige, waliapishwa na Rais Magufuli, baada ya kubadilishana nafasi kutoka wizara moja na nyingine.
Prof. Kabudi alikuwa waziri wa katiba na sheria, huku Dk. Mahiga akitokea mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Prof. Kabudi hakutaja jina la mtu anayedai kuwa amekuwa akiisema vibaya nchi mbele ya jumuiya ya kimataifa.
Hata hivyo, mwanasiasa anayetajwa kuzunguuka mataifa mbalimbali kueleza mabaya ya serikali, ni Lissu na kwamba mara kadhaa, ameyooshewa kidole na viongozi wa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwa anaichafua nchi mbele ya uso wa dunia.
Akiwageukia nchi wahisani, Prof. Kabudi alisema, “yeyote anakaribishwa kwenye nchi hii ili tufanye naye kazi.
Aliongeza, “mwenye matatizo na Tanzania, milango iko wazi na anakaribishwa kueleza matatizo yake.”
Akijibu madai hayo ya Prof. Kabudi, Lissu anasema, huyu ni profesa wa sheria, anayeelekea kutokufahamu au kuamini matakwa ya Katiba na Sheria za nchi yetu.
Anasema, “Nchi’ ya Tanzania ni ile inayotamkwa kwenye Ibara ya 1 na 2(1) ya Katiba kuwa “… ni Jamhuri ya Muungano (inayojumuisha) … eneo lote la Tanzania Bara na eneo lote la Tanzania Zanzibar, na ni pamoja na sehemu yake ya bahari ambayo Tanzania inapakana nayo.”
Kwa upande mwingine, serikali Tanzania imefafanuliwa katika ibara ya 6 ya Katiba. Inasema, “… ni pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Serikali za mitaa na pia mtu anayetekeleza madaraka au mamlaka yoyote kwa niaba ya Serikali yoyote.”
Hivyo basi, Lissu anasema, “matendo maovu ya vyombo vya usalama kama Jeshi la Polisi au Idara ya Usalama wa Taifa na Ujasusi; au ya viongozi wa serikali kama Rais, Mawaziri au Wakuu wa Mikoa na Wilaya; au watendaji wake wengine, sio matendo ya Nchi bali ni matendo ya Serikali.”
Kwa muktadha huo, Lissu anafafanua kuwa “matendo haya ya serikali yanaweza yakapingwa, kubezwa, kubagazwa, kusemwa vibaya au kuchafuliwa bila kuichafua au kuibeza au kuibagaza Nchi.”
Lissu anasema, “kuisema Serikali vibaya, au kuibagaza, au kuichafua – ndani au nje ya nchi – kwa sababu ya matendo yake maovu, sio kosa bali ni wajibu wa kila mtu na hasa kila raia wa Tanzania.”
“Kwa mujibu wa Ibara ya 3(1) ya Katiba yetu, Tanzania ni nchi ya kidemokrasia; yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa. Siyo nchi ya chama kimoja kama ilivyokuwa zamani, kwa hiyo kuipinga au kuikosoa Serikali iliyoko madarakani sio kosa, bali ni kutekeleza matakwa ya Katiba,” anafafanua.
Lissu ambaye amepata kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) anasema, “kwa mujibu wa Ibara ya 8(1)(a) , wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi….”
Aidha, ibara ya 8(1)(c) inasisitiza kwamba “Serikali itawajibika kwa wananchi.” Kwa maana hiyo, Lissu anasema, “sisi wananchi ndio tuko juu ya Serikali.
Anaongeza, “kuipinga, kuisema vibaya, kuibagaza au kuichafua serikali hiyo kutokana na matendo yake maovu, hakuwezi kuwa kosa hata kidogo, bali ni sehemu ya kuiwajibisha kwetu.”
Amemtaka Prof. Kabudi kuelewa kuwa serikali ina wajibu mbele ya jumuiya ya kimataifa wa kuheshimu haki za binadamu zilizoainishwa kwenye Katiba yetu.
Anasema, Ibara ya 9(f) ya Katiba inaitaka “… Mamlaka ya Nchi na vyombo vyake vyote … kuelekeza sera na shughuli zake zote katika lengo la kuhakikisha … kwamba heshima ya binadamu inahifadhiwa na kudumishwa kwa kufuata Kanuni za Tangazo la Dunia kuhusu Haki za Binadamu.”
Anasema, serikali imesaini mikataba mbali mbali ya kimataifa na ya kikanda inayoilazimisha kuheshimu haki za binadamu za wananchi wake; serikali imekubali, kwa kusaini Mkataba wa Roma unaounda Mahakama ya Kimataifa ya Jinai.
Kupitia mkataba huo, serikali imeahidi itawajibika kwa jumuiya ya kimataifa kwa vitendo vyovyote vya ukiukwaji wa haki za binadamu vilivyokatazwa na Mkataba wa Roma.
“Kama sehemu ya uwajibikaji wetu mbele ya jumuiya ya kimataifa kuhusu masuala ya haki za binadamu, Lissu anasema, “Serikali yetu inatakiwa kupeleka taarifa ya utekelezaji wa wajibu wake huo kwenye vyombo vya uwajibikaji vya kimataifa, kama vile Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa.
“Hivi ndivyo alivyofanya Profesa Kabudi mwenyewe wiki iliyopita kule Geneva, Uswisi.
“Kwa sababu hiyo, kuisema vibaya Serikali yetu nje ya Tanzania, kwa sababu ya matendo yake maovu dhidi ya Watanzania, ni sehemu tu ya kuitaka Serikali yetu iwajibike kwa jumuiya ya kimataifa kwa mambo ambayo tumekubali kuwajibika nayo kimataifa. Katiba yetu imetupatia Haki ya Uhuru wa Mawazo na Uhuru wa Maoni.
“Kwa mujibu wa Ibara ya 18(1), kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.”
Kwa sababu zote hizi, kama Prof. Kabudi yeye na serikali anayoitumikia hawaamini matakwa haya ya Katiba yetu, sisi tunayaamini na tutayatekeleza matakwa hayo.”
Akizungumzia kunyamzishwa na kauli hiyo, Lissu anasema, “mwambieni Prof. Kabudi, kwamba hatutanyamazishwa na uovu wao, au vitisho vyao, au na ulaghai na propaganda zao, au na hongo na rushwa zao. Tutaendelea kuyasema hadharani, popote pale, ndani na nje ya Tanzania, maovu ya Serikali yetu, na ya vyombo vyake, na ya viongozi wake na ya watendaji wake.”
Maelezo ya Lissu yako kwenye andishi lake alilolisambaza kwenye mitandao kadhaa ya kijamii na ambalo limethibitishwa na yeye mwenyewe kuwa ni lake.
Katika siku za hivi karibuni, Lissu ambaye yuko kwenye matibabu nchini Ubelgiji, amefanya mikutano na watu mbalimbali katika nchi za Ubelgiji, Ujerumani, Marekani na Uingereza.
Amefanya mahojiano pia na vyombo kadhaa vya habari vya kimataifa, akiituhumu na kuishutumu Serikali ya Rais Magufuli, kuminya uhuru wa kujieleza na kuvunja misingi ya kidemokrasia.
Lissu yuko nchini Ubelgiji, tokea 6 Januari 2018, kufuatia kushambuliwa kwa risasi na wanaoitwa na serikali, “watu wasiofahamika,” nje ya nyumba yake, Area D, mjini Dodoma.
Shambulio dhidi ya Lissu lilitokea tarehe 7 Septemba 2017, muda mfupi baada ya kushiriki mkutano wa Bunge wa asubuhi na kulihutubia Bunge.
No comments