Breaking News

Meatu watakiwa kukamilisha ujenzi wa wodi za akina mama na watoto



Na Mathew Kwembe, Simiyu

Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu umepewa hadi tarehe 30 machi, 2019 uhakikishe kuwa unakamilisha ujenzi wa majengo ya wodi ya akina mama na watoto ili huduma za matibabu katika zahanati na vituo vya afya wilayani humo ziweze kuanza mara moja.

Wito huo umetolewa jana na Mratibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani (UNFPA) kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Dinah Atinda wakati alipoongoza timu ya ufuatiliaji kwenye miradi ya ujenzi wa majengo ya wodi ya akina mama na watoto katika halmashauri hiyo.

Katika ziara hiyo, timu ya ufuatiliaji kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI ilibaini kuwa majengo yote ya akina mama na watoto katika zahanati za Bulyashi, Mwabulutago, Sakasaka, Kisesa, na Itinje hayajaanza kutoa huduma kwa akina mama ya kujifungulia kwa vile hayajakamilika.

Kufuatia hali hiyo Mratibu huyo wa UNFPA kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI alieleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu ihakikishe kuwa inayakamilisha majengo hayo ili akina mama na watoto waweze kuyatumia kwa ajili ya kupata matibabu.

Bi Atinda aliyataja baadhi ya mapungufu ya majengo hayo kuwa ni pamoja na baadhi yake kutokamilika sehemu ya vyoo, kutowekewa madirisha, na baadhi yake kuwa na milango mibovu na haina vitasa.

Mbali na changamoto hizo, Bi Atinda aliongeza kuwa baadhi ya zahanati zilikuwa zinakabiliwa na tatizo la kukosa maji ya uhakika na pia baadhi ya majengo vifaa vilivyotolewa na wafadhili UNFPA vilikuwa havijawekwa ndani ya majengo hayo.

Baada ya kuona changamoto hizo, Mratibu wa UNFPA kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Bi Atinda aliagiza halmashauri ya wilaya ya Meatu ihakikishe kuwa majengo hayo yanakamilika kabla ya tarehe 30 mwezi huu.

“Hakikisheni majengo haya yanakamilika kwa wakati, fanyeni kila muwezalo fedha itoke mkoani au katika halmashauri ili majengo haya yakamilike,” alifafanua bi Atinda.

Kwa upande wake Mhasibu kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI bwana Alex Lyimo alieleza kuwa kila zahanati katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu ilipewa shilingi milioni 30 kwa ajili ya kukamilisha jengo la akina mama na watoto kwa zahanati na shilingi milioni 450 kwa kila kituo cha afya katika wilaya zote za mkoa wa Simiyu.

Katika mchanguo wa fedha hizo kiasi cha shilingi milioni 250 zilitolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani (UNFPA) na shilingi milioni 200 zilitolewa na Serikali chini ya ufadhili wa nchi ya Denmark

Bwana Lyimo aliongeza kuwa halmashauri zote zilitakiwa kujenga majengo hayo kupitia mfumo wa ‘force account’ na hivyo kuhakikisha kuwa majengo hayo yanajengwa kwa ubora uliokusudiwa na bila kusababisha upotevu wa fedha.

Naye Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Meatu bwana John Kunguku aliyapokea maagizo hayo na kuongeza kuwa changamoto hiyo imetokana na tathmini ya Mhandisi wa ujenzi wa wilaya kuonyesha kuwa majengo hayo yangejengwa kwa kiasi hicho na kukamilika bila tatizo lolote.

Jumla ya vituo vya afya na zahanati 38 zilipewa fedha katika mkoa wa Simiyu kwa ajili ya kuboresha huduma za akina mama na watoto, fedha ambazo zilitolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani (UNFPA) kupitia shirika la misaada la Korea (KOICA) na pia ufadhili wa Serikali ya Denmark

No comments