Uchaguzi Yanga sasa Machi 10
NA ZAITUNI KIBWANA
UCHAGUZI Mkuu wa klabu ya Yanga uliosimamishwa siku mbili kabla ya tarehe iliyopangwa kufanyika Januari 13, kutokana na baadhi ya wanachama kukimbilia mahakamani, sasa utafanyika Machi 10 mwaka huu.
Uchaguzi huo ulisimamishwa baada ya baadhi ya wanachama kuweka pingamizi mahakamani katika mikoa mbalimbali ikiwemo Mbeya, Iringa, Morogoro na Dar es Salaam.
Habari za ndani ambazo gazeti hili lilizipata zinasema viongozi wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wenzao wa Kamati ya Yanga, wamekubaliana kwa pamoja kufanyika uchaguzi huo kwa tarehe hiyo.
“Tumekubaliana kwa pamoja yaani Kamati ya TFF na ile ya Yanga, kwanza tumeondoa tofauti zetu hivyo sasa uchaguzi huu utafanyika Machi 10 mwaka huu,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Wakati chanzo hicho kikisema hayo, BINGWA lilimtafuta Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Ally Mchungahela ambaye aligoma kukiri tarehe hiyo kwa kusema leo watakutana na kamati mpya ya Yanga kujadili kwa pamoja uchaguzi huo.
“Nipo njiani nakuja Dar es Salaam kwa ajili ya mkutano wa pamoja na viongozi wa Yanga, tutakaokutana kesho (leo) hivyo baada ya hapo ndipo itajulikana nini tumekiamua,” alisema.
Awali, uongozi wa Yanga uliunda kamati mpya ya uchaguzi mdogo ikiongozwa na wabunge wanne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kamati hiyo Mwenyekiti wake ni Venance Mwamoto ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kilolo, mkoani Iringa, Katibu wake ni Mbunge wa Jimbo la Manonga mkoani Tabora, Seif Gulamali, Dunstan Kitandula ambaye ni Mbunge wa Mkinga na Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Saidi Mtanda.
Uchaguzi huo ambao ni wa kujaza nafasi zilizoachwa wazi ikiwemo nafasi ya Mwenyekiti, Yussuph Manji aliyejiuzulu, umekuwa ukipigwa danadana kutokana na kuingia mkanganyiko kuhusu nafasi yake igombewe au isigombewe.
Hata hivyo, tayari wagombea mbalimbali walishajitokeza kugombea kabla ya kuahirishwa uchaguzi huo.
Nafasi ya Mwenyekiti inawaniwa na Dk. Jonas Tiboroha, Mbaraka Hussein Igangula na Erick Ninga.
Makamu Mwenyekiti wagombea ni Yono Kevela, Titus Osoro na Salum Magege.
Wakati nafasi nne za wajumbe wa Kamati ya Utendaji zinawaniwa na Hamad Islam, Benjamin Mwakasonda, Sylvestre Haule, Salim Seif, Shafil Amri, Said Kambi, Dominick Francis, Seko Jihadhari, Ally Omar Msigwa, Arafat Ally Hajji, Frank Kalokola, Ramadhani Said, Leonard Marango, Bernard Faustin Mabula, Christopher Kashiririka na Athanas Peter Kazige.
No comments