WAZIRI UMMY ANG’AKA MIKOPO KIDUCHU KWA WANAWAK
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amepiga marufuku mikopo ya laki tano kwa wanawake nchini bali wawezeshwe kupata mikopo yenye tija ili kuwa na uwezo wa kujikwamua kiuchumi.
Ameyasema hayo leo mkoani Mwanza alipokuwa akizungumza na Wanawake na wananchi wa Mkoa wa Mwanza katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Waziri Ummy Mwalimu amesema lengo la kuadhimisha Siku ya Wanawake katika nagzi ya mikoa kwa miaka mitano ni kutoa nafasi ya kujitathimini katika utekelezaji wa masuala mbalimbali kuhusu hali ya ka Maendeleo ya mwanamke.
Amesema kauli mbiu ya Siku ya Wanawake Duniani kwa mwaka 2019 inasema “Badili Fikra Kufikia Ustawi wa Kijinsia kwa Maendeleo Endelevu” Kauli mbiu hii isaidie kubadili fikra katika kuhakikisha tunafikia uchumi wa viwanda kwa kutoa umuhimu kwa mwanamke, mwanaume na taifa zima ili kuona ni kwa jinsi gani ataweza kushiriki katika kulifanikisha hilo.
Amemuagiza Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia Bw. Julius Mbilinyi kuhakikisha Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wanatoa taarifa za kila robo mwaka za utoaji wa mikopo inayotolewa kwa vikundi mbalimbali katika kila mkoa husika.
“Nimesikitishwa na utoaji mikopo kwa wanawake maana nimetembelea kikundi cha Wanawake kwenye mabanda chenye watu 30 lakini wamepatiwa mkopo wa milioni moja ambao hauna tija kulingana na idadi ya wanachama hao” alisema.
Amesema kuwa ushiriki wa wanaume ni muhimu katika kufikia suala la kijinsia na maendeleo endelevu katika Taifa letu kwani wanaume ni sehemu kubwa katika kuwezesha mwanamke kiuchumi.
Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano iliandaa na kutekeleza Mpango Mkazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto zikiwemo mimba na ndoa za utotoni ambazo ni kikwazo kwa Maendeleo ya wanawake na Mtoto wa kike nchini.
Serikali imeendelea kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kutoka Bilioni 8 mwaka 2015 hadi Bilioni 16 kwa mwaka 2017/18 kiasi ambacho ni mara mbili zaidi hivyo kuongeza nguvu katika kumuwezesha mwanamke kiuchumi.
Amewataka wanawake kundokana na unyonge uliopo na kusimama na kujitoa na kupambana hasa katika kugombea nafasi za maamuzi katika uongozi na pia kupendana na kuinuana katika kupeana taarifa na fursa mbalimbali za kimaendeleo.
Aidha ameitaka jamii katika maeneo ya kazi kuondokana na rushwa za ngono jambo ambalo ni tatizo katika upatikanaji wa haki za wanawake na waajiri wa Sekta za Binafsi ni muhimu kuzingatia usalama na haki za wanawake wafanyakazi.
Akimkaribisha mgeni rasmi Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Philis Nyimbi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana amesema mkoa unatekeleza mikakati mbalimbali katika kumuwezesha Mwanamke na Mtoto wa kike kwa kumuweka mbali na Vitendo vya Ukatili dhidi yao ili kuwawezesha kupata fursa zitakazowezesha kufikia usawa wa kijinsia.
Ameongeza kuwa Mkoa unaendelea na Kampeni za kutoa elimu kwa wananchi katika suala zina la kupinga Ukatili dhidi ya wanawake na watoto ikiwa ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Kitaifa wa kutokomeza vitendo hivyo.
“Katika kutekeleza Mpango Mkakati wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto kwa kuanzisha Kamati za ulinzi wa Mwanamke na Mtoto kuanzia ngazi ya Mkoa, Halmashauri, Kata, Mitaa na Vijiji na kuimarisha utendaji wake ili zisaidie kupambana na Vitendo vya Ukatili katika sehemu zao” alisema.
Akitoa Salamu kwa Wanawake Mbunge wa Ilemela na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angelina Mabula amesema kuwa katika Siku hii mwanamke anatakiwa kujitambua na ni wakati wa wanawake kusimama na kufanya Maendeleo na mwanamke asiyesimama imara mambo mengi huharibika na wanayofursa za kuunga mkono juhudi za mapambano ya kumuwezesha mwanamke.
“Tushikamane mikono wenyewe kwa wenyewe tujikombe sisi kama wanawake ili kuondokana na ukandamizaji na kusisimama na kuwa na sauti moja ili kujiletea Maendeleo yenye fikra chanya” alisema
Naye Mwakilishi Mkazi Umoja wa Mataifa Bw. Alvaro Rodriguez amesema kuwa Umoja wa Mataifa unataendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kwa kuhakikisha kunakuwepo na usawa wa kijinsia na kuondoa vikwazo vyote vinavyosababisha kutokuwepo kwa usawa wa kijinsia kama vile mimba na ndoa za utotoni ambazo zimekuwa zikiwanyima fursa watoto wa kike kutimiza ndoto zao.
Ameongeza kuwa mapambano ya usawa wa kijinsia yatafanikiwa pale yatakaposhirikisha wanaume na wavulana katika kuhakikisha wasichana na Wanawake wanapata fursa sawa katika kutikiza ndoto zao.
Kwa upande wake Mwakikishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake UN Women Bi. Hodan Addou amesema kuwa Shirika hilo linashirikiana na Serikali na Mashirika ya kitaifa kuhakikisha elimu inatolewa na usawa wa kijinsia unakuwa suala la kipaumbele katika Jamii zetu.
Akizungumzia kuhusu Kampeni ya Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto msanii Nurdin Bilal maarufu kama Shetta amesema lengo la Kampeni hiyo ni kubadili fikra wanaume ambao ni watendaji wakubwa vitendo vya Ukatili Dhidi ya wanawake na Watoto.
Ameongeza kuwa Ukatili wa kijinsia hauathiri wanawake pekee bali hata wale ambao wanaowazunguka hasa Watoto hivyo amewaasa wanaume kuachana na vitendo vya kikatili kwa wanawake.
“Mimi nina amini ukimthamini Mwanamke unaleta maendeleo katika Taifa kwani mwanamke ni nguzo ya Maendeleo kwa Taifa” alisema.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Wanawake Mkoa wa Mwanza Bi. Grace Bunyinyiga amesema kuwa bado mwanamke ana vikwazo vingi katika kuleta chachu ya Maendeleo na kuna haja ya kuwakomboa wanawake wenyewe kifijra wawe mabadiliko katika Jamii husika.
“Wanawake wa Mkoa wa Mwanza wawe kipaumbele katika kuhakikisha uwepo wa usawa wa kijinsia katika Jamii zao na ushiriki wa wanaume na kuondokana na mila na desturi zilizopitwa na wakati ili kuondokana na vitendo vya kikatili” alisema
Katika Maadhimisho hayo Waziri Ummy Mwalimu alizindua Kampeni ya Kupambana na kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto ijulikanayo kama SAWA inayoratibiwa na Msanii SHETTA

No comments