Breaking News

JE UNAJUA JINA ZURI LA KUMUITA MPENZI WAKO?



KATIKA kila jamii, yapo majina ya kumwita mtu ambaye unashirikina naye kimapenzi, au pengine una mpango wa kuwa naye katika maisha yako ya baadaye.

Majina haya hutofautiana kwa kuzingatia muktadha na kwa kuzingatiwa mtu anayetambulishwa. Ni wazi kuwa jinsi utakavyomtambulisha 'demu' wako kwa rafiki yako, sivyo utakavyomtambulisha kwa ndugu yako unayemheshimu.

Majina haya ya utambulisho huanza kutumika mapema kwa kadri watu wanavyozoeana. Inatokea kwamba umeshampata mtu uliyekuwa unamtafuta, au angalau mwenye sifa zinazokaribiana na za yule uliyekuwa ukimwota utotoni mwako.



Yawezekana ikawa ni wiki sita tu tangu mlipoonana kwa mara ya kwanza, au hata siku kadhaa tangu alipokutamkia kuwa yuko tayari kuwa nawe katika suala zima la mapenzi au uchumba.

Mara nyingi katika hatua hii, kila mmoja atakuwa na mawazo na ndoto kuwa yamkini huyo mwenzake atakuwa mtu muhimu sana maishani mwake, kwamba mathalani, ndiye atakuwa baba au mama wa watoto wake.

Haya ni mawazo mazuri, kwani yakiendelezwa ndiyo baadaye huleta heshima, ambayo husababisha kukua kwa uhusiano na baadaye wapenzi kutimiza ndoto zao za kuishi pamoja kama watoto wawili wapendanao.

Kadiri muda unavyokwenda, ni wazi kuwa utakuwa na haja ya kumtambulisha mwenzio kwa ndugu, jamaa na marafiki zako, au hata mfanyakazi mwenzako ambaye unaamini anapaswa kuwa miongoni mwa watu wa kwanza kufahamu uhusiano wenu.

Utambulisho huo unaweza kuwa rasmi, mathalani umealikwa kwenye hafla halafu ukaenda naye, ni wazi itabidi uwaeleze wale wanaokufahamu huyo uliyeingia naye ni nani.

Lakini pia inaweza kuwa katika mazungumzo ya kawaida, mathalani mara kwa mara umekuwa ukionekana ukiwa na mtu huyo karibu na sasa watu wanataka kufahamu mna uhusiano gani.

Je, utamwita boyfriend au girlfriend, majina ya Kiingereza ambayo yamekuwa maarufu miongoni mwa vijana katika zama hizi? Je, utamwita mwenza? Je, utamtambulisha kama mpenzi wako? Je, utasema ni rafiki yako? Au utasema ni mfanyakazi mwenzako?

Mara nyingi hili ni suala ambalo huwasumbua watu wengi na wengi husita kwanza kabla hawajatoa majibu. Sababu kubwa ya kusita huku hutokana na ukweli kwamba, mtu anakuwa hajafahamu kwa uhakika ni nini utakuwa mustakabali wa uhusiano wake na mwenzake.

Lakini pia, yapo maneno mbalimbali yanayoweza kutumika kumtambulisha mwenzako, ila yote yana maana tofauti, hivyo kusababisha ugumu katika uchaguzi.

Hata hivyo, hakuna haja ya kuwa na wasiwasi. Unapaswa kuwa huru na kutumia neno ambalo kweli umelimaanisha, ili hata kama baadaye mwenzako ataamua kuachana nawe, aibu iwe kwake, kwani wewe ulishaonesha wazi msimamo wako hata kwa ndugu, jamaa na marafiki.

UTAMWITA MWENZA/MWENZI?

Katika hatua fulani ya uhusiano baina ya mwanamke na mwanaume, hufikia wakati wakawa wanaitana wenza (au wenzi).

Neno 'mwenza' au 'mwenzi' katika Kiswahili lina maana ya 'rafiki', lakini hapa maana yake hupanuliwa zaidi, likamaanisha kuwa ni mtu ambaye mko pamoja, pengine ni mke au mume.

Hata hivyo, neno hili linaweza kupunguza uzito katika suala zima la mapenzi, ikadhaniwa kuwa pengine huyo ni rafiki wa kawaida, au ni mbia wako katika biashara. Hizo maana za ziada zinaweza kumjia mpenzi wako akitambulishwa hivyo na pengine akakwazika.

Kwa sababu hiyo, inapendeza zaidi kumwita 'mwenza' au 'mwenzi' mtu ambaye tayari unaishi naye, ama kama mke na mume, au kama bwana na bibi, lakini si wiki mbili tu tangu mlipoanza kutamkiana maneno ya kupendana.

Ni neno ambalo hufaa kutumika wakati ambapo wapenzi wanaishi kwa kutegemeana, tena pengine wameshafunga ndoa na wana watoto, lakini si wakati wa kutongozana - wakati ambapo hakuna anayefahamu mustakabali wa uhusiano unaohusika.

UTAMWITA GIRLFRIEND/BOYFRIEND?

Kama kumwita mpenzi wako 'mwenza' inatisha, basi inaweza kuwa rahisi zaidi kumwita 'boyfriend' au 'girlfriend'.

Hata hivyo, hii inaweza ikakufanya ujihisi kuwa unafanya utoto, hasa kama unahisi kuwa umri wako umeendelea kidogo, lakini kwa ujumla hayana maana mbaya.

Pia jina la 'girlfriend' au 'boyfriend' linaweza kusababisha matatizo kidogo katika jamii zetu za kiafrika, kwani mara nyingi watu hawapendi kujionesha kuwa wanapendana, bali hutaka kuwashtukiza watu kwa kadi za michango ya harusi.

Kwa hiyo, matumizi ya jina hilo yatategemea watu ambao unamtambulisha mpenzi wao kwako. Kama ni marafiki wa kawaida unaweza usiwe na wasiwasi, isipokuwa unapaswa kuwa makini kwa ndugu, hasa waliokuzidi kiumri, kwani kwa mila zetu bado inadhaniwa kuwa mtu hapaswi kuwa na mpenzi kabla ya ndoa.

UTASEMA NI MCHUMBA?

Neno 'mchumba' halina matatizo, lakini linapotamkwa humaanisha kuwa una uhakika kuwa huyo uliye naye ndiye baadaye atakuwa mama/baba wa watoto wako.

Sasa hapa itabidi ujiulize, je, kweli tumekubaliana kuwa wachumba? Je, alishakuvalisha pete ya uchumba? Kama ni mwanaume alishaleta posa kwenu? Au kama wewe ni mwanaume unamaanisha kweli kuwa utamwoa?

Mara nyingi msichana ndiye anayepaswa kuwa makini na neno hili, kwani wengi wao hudanganywa na hata kuvalishwa pete, kisha kuachwa 'kwenye mataa' na wanaume waliokuwa na malengo ya kumfaidi tu.

UTAMWITA MPENZI/RAFIKI?

Kama mmekuwa pamoja kwa muda mfupi tu na hamjapeana ahadi zozote za uchumba na pengine ukawa hujafahamu hata majina yake yote, ni vema tu ukasema, 'huyu ni rafiki yangu'.

'Rafiki' ni neno lisilo na matatizo na ni la heshima. Kubali tu kuwa kwa kipindi fulani ataendelea kuwa rafiki yako, mpaka pale mtakapokubaliana kuhusiana na masuala mengine makubwa ya kimaisha.

Haipendezi mnapokuwa na watu wenye heshima zao, mwanaume kumtambulisha mwanamke kama 'demu', kwani ni neno la mitaani zaidi. Kama unajihisi huru katika mambo yako na hutarajiwi kuulizwa na mtu, basi ni vema kumwita 'mpenzi'.

Neno 'mpenzi' halikufungi sana. Ipo mifano mingi ya mapenzi yaliyokwama, kwa hiyo hata kama baadaye watu watasikia kuwa mmeachana hakutakuwa na tatizo, kwani kuachana ni jambo la kawaida.

Lakini ukisema 'mchumba', siku nyingine ukikutana na ndugu au rafiki yako ukamtambulisha kwa mchumba mwingine baada ya yule wa kwanza kukuacha, hatakuelewa na atakuona kama mtu mwenye kuingia kwenye mapenzi kwa papara.

Kwa ujumla, unaweza kutumia maneno yoyote kumtambulisha mwenzako, kwa kuzingatia hatua ambayo tayari mmeipiga, pamoja na heshima uliyo nayo kwake. Lakini la msingi ni kuhakikisha kuwa humkwazi yeyote katika utambulisho wako.

Maoni 0685-290000 aumgosius@yahoo.com

No comments