MAKAMU WA RAIS MAMA SAMIA AMPA UJUMBE DC WA TARIME

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Tarime, aliyeapishwa na Rais Magufuli siku ya jana kuhakikisha anazifanyia kazi mila na desturi za huko Tarime haswa zile zinazowakandamiza wanawake na watoto.
Samia ameyasema hayo baada ya Rais kuwaapisha majaji 15 wa Mahakama Kuu na sita wa Mahakama ya Rufani, Pia, wakurugenzi 10 wa halmashauri na wakuu hao wa wilaya wapya walioteuliwa Januari 27, 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mkuu huyo wa wilaya mpya wa Tarime ambaye alikuwa kiongozi wa mbio za mwenge 2018, Charles Kabeho ameagizwa kutorudia makosa yaliyofanywa na kiongozi aliyepita huku akitahadharishwa na kiongozi huyo kuhusu changamoto ya rushwa.
“Watu wa Tarime wanafahamika jinsi walivyo, wewe nenda ukafanye kazi. Kule kuna changamoto ya rushwa, nenda ukashughulikie. Zile mila na desturi mbovu za unyanyasaji wa wanawake, watoto tafadhali zifanyie kazi ziondoke, zile nzuri ziache na kwa upande wa wakurugenzi nanyi fanyeni kazi hivyohivyo,” amesema Samia.
Hata hivyo, Mh. Suluhu ameongeza kwamba, “ni imani yangu aliyepangwa Mwanga atakwenda kurekebisha hayo kwa sababu imekuwa ikikosa maendeleo kwa sababu ya uongozi mbaya na haufanyi kazi vizuri,” ameongeza.
No comments