Breaking News

Yanga Yapigwa 3-2 Yatupwa Nje Sportpesa Super Cup



Kikosi cha Yanga kimeondolewa katika mashindano ya SportPesa dhidi ya Kariobangi Sharks ya Kenya baada ya kupokea kichapo cha mabao 3-2, mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Yanga ambayo imeyaaga mashindano hayo walipata mabao hayo mawili kupitia kwa Mrundi Amissi Tambwe dakika ya 87 na Mkongo Haritier Makambo ndani ya dakika za nyongeza baada ya 90, kumalizika.
Kariobangi Sharks wao walifunga mabao yao kupitia kwa Abuya Duke
aliyepachika mawili la kwanza dakika ya 9 na la tatu dakika za nyongeza baada ya 90, kumalizika huku Abege George akipiga la pili dakika 36.
Mchezo huo ambao ulikuwa wa pili baada ya wa kwanza ambao  Singida United waliondoshwa katika mashindano hayo yaliyoanza kutimua vumbi rasmi leo Jumanne na Bandari FC kutoka Kenya.
Yanga ikiwa chini ya Kocha Mcongo Mwinyi Zahera walianza na kikosi kamili cha wachezaji ambao huwatumia mara kwa mara katika mechi zao za Ligi Kuu Bara.
Walicheza kwa kujiamini lakini muda mwingi walizidiwa na kutawaliwa katika kumiliki mpira, Sharks wao walionekana kumiliki mpira na kutengeneza nafasi nyingi ambazo kama wangekuwa makini wangefunga mabao mengi.
Ndani ya dakika za nyongeza kabla ya mchezo kumalizika Yanga wakiwa wametoka kufunga bao la pili ilitokea vurugu ya maana.
Vurugu hiyo ilitokana na kipa wa Kariobangi Sharks, Onyamba John kung'ang'ania mpira akiwa ndani golini. Vurugu hizi zilionekana kwa wachezaji wa timu zote mbili kupigana na kurushiana ngumi na mateke.
Mara baada ya mwamuzi, George Gatogato kupiga kipyenga cha mwisho kuamuru kumalizika kwa mechi maskari na walinzi walionekana kuwalinda waamuzi hao wakiwa wanaenda vyumbani.
Msimu wa uliopita wa mashindano haya yakichezwa nchini Kenya Yanga waliishia katika hatua ya awali wakifungwa dhidi ya Kakamega Home Boys.

No comments