Breaking News

Wanawake nchini watakiwa kudumisha umoja na upendo katika jamii


Wanawake nchini wametakiwa kudumisha umoja na upendo baina yao ili kufikia mafanikio na maendeleo ya kuinua uchumi mwaamke wa kitanzania.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri, Sera, Bunge, Kazi,, Vijana, Ajira na Walemavu Mhe. Anthony Mavunde kwenye maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani iliyofanyika jana Kimkoa katika viwanja vya Mashujaa Jijini Dodoma.

Mhe. Mavunde amesema kuwa wakinamama wakidumisha umoja na mshikamano wataleta chachu katika kupigania haki za mwanamke na kuleta fikra pevu ndani ya jamii ya kitanzania.

Ameendelea kusema kuwa wanawake wanatakiwa kuwa na malengo makubwa zaidi bila kusahau majukum yao katika ngazi ya familia kwa kuwa wao ndio kiungo muhimu katika malezi, maendeleo na mafanikio ndani ya jamii.

Naye Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Dorothy Gwajima amesema kuwa wanawake wanatakiwa kuwa na udhubutu katika ngazi yeyote ile anayopangiwa kimadaraka japo kuna changamoto mbalimbali katika jamii lakini wanahitajika kuwa jasiri katika kufikia malengo na kuleta maendeleo kwa kuanzia ngazi ya familia, jamii na taifa kwa ujumla.

“Ili mwanamke aweze kudhubutu lazima apatiwe elimu itakayomuwezesha kufanikisha malengo yake aliyojiwekea katika jamii, hasa ukizingatia kuwa mwanamke ndio muhimili mkuu kuanzia ngazi ya familia, jamii na Taifa kwa ujumla katika kuleta maendeleo endelevu. ” Amesema Dkt. Gwajima

Dkt Gwajima ameongeza kuwa mwanamke akijitambua katika nafasi yake kwenye jamii basi hicho ni kiashiria tosha kinachoonyesha kuwa yeye ni jasiri na anawezaa kusimama na kupewa haki sawa bila kubaguliwa katika jamii inayomzunguka.

Amesema kuwa katika kutafakari maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani inapaswa kutafakari changamoto na mafanikio yaliyokwishapatikana tangu maadhimisho hayo yalipoanza kufanyika kwa kuwa na takwimu sahihi zinazoonyesha mafanikio yaliyopatikana kwa wananwake na jamii kwa ujumla.

Dkt. Gwajima ameendelea kufafanua ni vyema mabadiliko ya fikra yakaanzia ngazi ya Menejimenti mbalimbali za Serikali kwa kuchambua sera zilizopo katika kuleta usawa ndani ya jamii na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Mhasibu kutoka Ofisi ya Rais,TAMISEMI Bi.Rose Makange ametoa wito kwa wanawake wote nchini kutumia vikundi vya wanawake vizuri ili kuwa na mafanikio endelevu.

“Wanawake wanatakiwa kubadili fikra zao kwa kudumisha upendo na mshikamano ili mwanamke wa kitanzania aweze kusimama imara na kuchangia katika kukuza uchumi wa nchi yetu” Amesema Bi. Makange.

Ameongezea kuwa umefika wakati wanawake kupitia vikundi vyao kubuni nini kifanyike katika kukuza pato la kikundi kwa kuanzisha miradi mbali mbali itakayo kuja kuwasaidia na kuwaletea maendeleo endelevu ndani ya jamii.

Aidha Maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani huadhimishwa kila tarehe 8 Machi kila mwaka ambapo wanawake wote duniani uazimisha siku hiyo ambapo kwa mwaka huu maadhimisho hayo yamefanyika kila Mkoa na Kaulimbinu ya mwaka huu ni “Badili fikra kufikia usawa wa jinsia kwa maendeleo endelevu.

No comments